Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 12 Oktoba, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
amewataka Watumishi wa Umma kuwa na utamaduni wa kufanya kazi kwa uadilifu bila
kushinikizwa wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kama ambavyo
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza.
Mhe. Mchengerwa
ametoa wito huo leo ofisini kwake, wakati wa mkutano wake na Waandishi wa Habari
uliolenga kutoa mrejesho wa masuala ya kiutumishi yaliyojitokeza wakati wa
ziara yake ya kikazi aliyoifanya hivi karibuni katika Mikoa ya Mwanza, Mara na
Simiyu.
Mhe. Mchengerwa
amesema, Mhe. Rais amedhamiria kuwa na watendaji waadilifu, hivyo ofisi yake
imejipajipanga kuhakikisha watumishi wote wa umma wanasimamia vema fedha
zinazotolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Ameongeza kuwa, Mhe.
Rais Samia Suluhu Hassan atajisikia fahari kuona Watumishi wa Umma wanatekeleza majukumu yao
kikamilifu bila kushinikizwa na viongozi wao.
“Inawezekana wapo
baadhi ya watumishi wanataka kutekeleza wajibu wao kwa kushinikizwa jambo
ambalo Mhe. Rais halitaki kwani anataka kila mtumishi awajibike bila kusimamiwa,”
Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Aidha, Mhe.
Mchengerwa amewataka Watumishi wa Umma nchini kuzingatia maelekezo ya Mhe. Rais
kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano
dhidi ya UVIKO 19 aliyoyatoa tarehe 10 Oktoba, 2021.
Amewaasa Watumishi wa
Umma kutekeleza mpango huo kwa weledi, uadilifu na uzalendo ili ukamilike kwa
wakati na kuwa na manufaa kwa wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
“Kama ambavyo Mhe.
Rais amesisitiza, muda wa utekelezaji wa mpango huo ni miezi 9 tu, hivyo
hakutakuwa na muda wa nyongeza,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.
Mhe. Mchengerwa amesema,
Watumishi wa Umma waliopewa dhamana ya kusimamia mradi huo wanapaswa kutekeleza
mradi kwa weledi na uzalendo ili kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere.
Mchango wa Watumishi wa Umma katika Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO ni muhimu kwa maendeleo na ustawi wa taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
(wapili kutoka kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo
jijini Dodoma kuhusu mrejesho wa masuala ya kiutumishi yaliyojitokeza wakati wa
ziara yake ya kikazi aliyoifanya katika Mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe.Deogratius Ndejembi (aliyesimama) akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
wakati wa kikao cha Mhe. Mchengerwa na Waandishi wa Habari kilichofanyika leo
jijini Dodoma kuhusu mrejesho wa masuala ya kiutumishi yaliyojitokeza wakati wa
ziara yake ya kikazi aliyoifanya katika Mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu.
Baadhi
ya Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza na Waandishi wa
Habari leo jijini Dodoma kuhusu mrejesho wa masuala ya kiutumishi yaliyojitokeza
wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya katika Mikoa ya Mwanza, Mara na
Simiyu.
Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro
(aliyesimama) akitoa neno la utangulizi kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
kuzungumnza na Waandishi wa Habari leo jijini Dodoma kuhusu mrejesho wa masuala
ya kiutumishi yaliyojitokeza wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya katika Mikoa
ya Mwanza, Mara na Simiyu.
No comments:
Post a Comment