Na. James
K. Mwanamyoto-Bariadi
Tarehe 08 Oktoba, 2021
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa amewataka Watumishi wa Umma nchini kuzingatia
Mwongozo wa Mavazi kwa Watumishi wa Umma kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa
Umma Na.6 wa Mwaka 2020 wanapokuwa mahala pa kazi wakitekeleza majukumu yao.
Mhe.
Mchengerwa ametoa wito huo leo mkoani Simiyu alipokuwa akizungumza na Watumishi
wa Umma wa Mkoa huo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa
Watumishi wa Umma mkoani humo.
Mhe.
Mchengerwa amesema, kuna baadhi ya Watumishi wa Umma katika taasisi mbalimbali za
umma hawazingatii Mwongozo huo, na badala yake wanavaa mavazi yasiyostahili
sehemu za kazi.
“Nawataka
Watumishi wote wa Umma nchini kuzingatia Mwongozo wa Mavazi kwa Watumishi wa
Umma kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Umma Na.6 wa Mwaka 2020 wanapokuwa
katika utekelezaji wa majukumu yao kwani kuna baadhi ya Watumishi hawauzingatii
Mwongozo huu na kuvaa wanavyojisikia wao, jambo hili sitaki kuliona,” Mhe.
Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa ameainisha kuwa, mwongozo huo unafafanua
aina ya mavazi yanayoruhusiwa na yasiyoruhusiwa kuvaliwa na Mtumishi wa Umma kulingana
na eneo alilopo wakati akitekeleza majukumu yake.
Aidha, Mhe.
Mchengerwa amewasisitiza watumishi kuacha matumizi ya simu wanapowahudumia
wateja kwani kwa kufanya hivyo wanawakatisha tamaa wananchi wanaofuata huduma
na kuijengea taswira mbaya Serikali kwa wananchi wake.
“Kuna baadhi
ya watumishi wamekuwa wakitumia simu na hata wakiona wateja bado wanaendelea
kufanya hivyo badala ya kuwahudumia, ninawataka muache tabia hiyo mara moja, tufanye
kazi kwa weledi, tujitoe kwa ajili ya wananchi, tuwasilikilize wananchi
wanapofuata huduma, tuwajali maana nchi hii ni yao na tupo kazini kwa ajili
yao,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe.
Mchengerwa yuko Mkoani Simiyu kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili kuhimiza
uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF
akitokea Mkoani Mwanza na Mara.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akisalimiana na Watendaji na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama wa Mkoa wa Simiyu alipowasili katika mkoani humo kwa ziara yake ya
kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Mkoa wa Simiyu
alipowasili katika Mkoa huo kwa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji
kwa Watumishi wa Umma.
Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu, Mhe. David Kafulila akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Mkoa wake
kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya
Mhe. Mchengerwa ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani Simiyu.
Mtumishi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Itilima, Bw. Haruna Taratibu akiwasilisha hoja ya kiutumishi kwa Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake
ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani Simiyu.
No comments:
Post a Comment