Na. James
K. Mwanamyoto-Maswa
Tarehe 09 Oktoba, 2021
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa amewataka baadhi ya Watendaji katika Taasisi za
Umma kutoendekeza fitina na majungu zinazowanyima fursa za uteuzi watumishi waadilifu
na wachapakazi.
Mhe.
Mchengerwa ametoa wito huo leo Wilayani Maswa alipokuwa akizungumza na Watendaji
na Viongozi wa Wilaya hiyo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza
uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Mhe.
Mchengerwa amesema, ili kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere tukiwa tunaelekea miaka 60 ya Uhuru wa nchi yetu, Watendaji na Viongozi
hawana budi kusimamia misingi ya haki ambayo Mwalimu Nyerere alituachia ili
kujenga taifa letu.
Mhe.
Mchengerwa amesema, kuna Watumishi wengi ambao ni waadilifu, wachapakazi wazuri
na wanastahili kupewa nafasi za uteuzi lakini kwa kuwa baadhi ya Watendaji
wanasikiliza majungu na fitina wanawaacha na kupewapendekeza wengine ambao
hawana sifa stahiki.
“Tutumie
vizuri nafasi za uongozi tulizopewa kwa kutenda haki badala ya kuendekeza fitina
na majungu na kuwakosesha haki watumishi wanaostahili na hatimaye kuwakatisha
tamaa ya kutekeleza kikamilifu majukumu yao,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Ili kupata
watumishi wenye sifa, amewataka Watendaji hao kujiridhisha na vigezo vya
utendaji kazi wa watumishi ambao majina yao wanayawasilisha Ofisi ya Rais-UTUMISHI
kwa ajili ya taratibu za uteuzi.
“Tutende
haki, tusiwasilishe majina ya nafasi za uteuzi kwa kigezo cha kufahamiana bali
tujiridhishe na utendaji kazi wa watumishi ambao majina yao yanawasilishwa
kwani kuna watumishi wengine hawana watu wanaowafahamu wa kuwasaidia na ni
wachapakazi wazuri sana, hivyo tusiwakatishe tamaa,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.
Kwa upande
wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi Prisca Kayombo amekiri kupokea maelekezo
ya Mhe. Waziri na kuahidi kusimamia vema utekelezaji wa maelekezo hayo.
“Mhe. Waziri,
tumeyapokea maelekezo yako, mimi nikiwa ndiye Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu,
nimeguswa sana na maelekezo yako, hivyo
nitahakikisha naweka usimamizi mzuri kwa Watumishi wa Umma wa Mkoa huu ikiwa ni
pamoja na kutenda haki kwa Watumishi wote,” Bibi. Kayombo amesisitiza.
Mhe.
Mchengerwa amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Simiyu
iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa
miradi ya TASAF.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akizungumza na Watendaji na Viongozi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Maswa alipowasili wilayani humo kwa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza
uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akisisitiza jambo kwa Watendaji na Viongozi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Maswa alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya
kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya
TASAF.
Katibu
Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi Prisca Kayombo akitoa neno la shukrani kwa Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa mara baada ya Mhe. Mchengerwa kuzungumza nao wakati wa ziara
ya kikazi ya Mhe. Mchengerwa ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma
Wilayani Maswa na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Mkuu wa
Wilaya ya Maswa, Mhe. Aswege Kaminyoge akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
Wilaya yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe.
Mchengerwa ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma Wilayani Maswa na
kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
No comments:
Post a Comment