Saturday, February 10, 2024

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI (PAC) YAIPONGEZA eGA KWA KULETA MABADILIKO KATIKA UTUMISHI WA UMMA

 Na. Rainer Budodi na Veronica Mwafisi – Dodoma

Tarehe 10 Februari, 2024

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Japhet Hasunga na wajumbe wa kamati yake wameipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia taasisi yake ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kuleta mabadiliko katika utumishi wa umma kupitia Mifumo ya TEHAMA ambayo imerahisisha upatikanaji wa huduma bora nchini.

Mhe. Hasunga ameyasema hayo leo wakati kamati yake ilipofanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) ambacho kipo chini ya Mamlaka ya Serikali Mtandao.

“Kamati yetu imefurahishwa sana na utendaji kazi wa wataalam wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na taasisi yake ya Mamlaka ya Serikali Mtandao eGA kwani haya yote tunayoyaona ni sehemu ya mabadiliko ya kuboresha utumishi wa umma nchini, kipindi cha nyuma haikuwa rahisi watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kupitia Mifumo ya TEHAMA,” Mhe. Hasunga amesema. 

Mhe. Hasunga ameipongeza eGA kwa jitihada kubwa inazofanya za kuunganisha mifumo ya TEHAMA iliyopo kwenye taasisi za umma ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwa wakati na mahali popote.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Kituo kinafanya utafiti na kubuni mifumo ya TEHAMA Serikalini yenye uwezo kuongeza kasi katika jitihada za utoaji wa huduma kwa umma kwa haraka na gharama nafuu.

Mhe. Kikwete ameishukuru Kamati kwa kupanga ziara hiyo muhimu katika  kituo  ambapo ushauri na maelekezo yamepokelewa na Ofisi yake iko tayari kusimamia utekelezaji wake ili wananchi waweze kunufaika na uwepo wa teknolojia.

Naye, Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amewahakikishia wajumbe wa kamati hiyo kuwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itaendelea kuisimamia Mamlaka ya Serikali Mtandao ili iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa lengo la kuboresha utoaji huduma bora kwa wananchi kupitia Mifumo ya TEHAMA.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Eng. Benedict Ndomba ameishukuru kamati hiyo kwa kufanya ziara ya kikazi katika kituo hicho na kuahidi kuendelea kubuni mifumo mbalimbali kwa maendeleo ya taifa.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe. Japhet Hasunga akizungumza na Viongozi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na watendaji wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wakati kamati hiyo ilipofanya ziara katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) jijini Dodoma. 

Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Eng. Benedict Ndomba (hayupo pichani) wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) jijini Dodoma

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete akitoa neno la utangulizi kwa   Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) jijini Dodoma. 


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akitoa neno la shukrani kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) mara baada ya kuhitimisha ziara katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Eng. Benedict Ndomba akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) walipofanya ziara katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) jijini Dodoma.


Mjumbe wa Kamati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhe.  Emmanuel Ole Shangai akichangia hoja kuhusu serikali mtandao wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (e-GovRIDC) jijini Dodoma.

 






Wednesday, February 7, 2024

MIPANGO YA TAASISI ITUMIKE KATIKA KUTATUA CHANGAMOTO YA URUDUFU WA MIFUMO YA TEHAMA-MHE.KIKWETE



Na. Veronica Mwafisi - Arusha

Tarehe 08 Februari, 2024

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amezielekeza taasisi zote za umma kuweka mipango itakayozisaidia kutatua changamoto ya urudufu wa mifumo ya TEHAMA ili kukuza na kuimarisha jitihada za serikali mtandao na kuboresha utendaji kazi katika kutoa huduma bora kwa wananchi kwa lengo la kufikia azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa na serikali ya kidijitali.

Mhe. Kikwete ametoa maelekezo hayo jijini Arusha wakati akifunga Kikao kazi cha nne cha serikali mtandao kilichowashirikisha wadau zaidi ya 1300 wa serikali mtandao nchini.

“Changamoto za TEHAMA ili ziweze kufikia mafanikio katika utekelezaji wa jitihada za serikali mtandao, hatua madhubuti zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kujiwekea mipango katika taasisi zenu ili changamoto hizo ziweze kutatuliwa,” Mhe. Kikwete amesisitiza.

Aidha Mhe. Kikwete amewataka wataalam wa TEHAMA kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika kutekeleza jitihada za serikali mtandao kupitia msaada na ushauri wa kitaalam unaotolewa na mamlaka hiyo kwa lengo la kila mtumishi kuweza kuijenga serikali ya kidijitali.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kutekeleza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuijenga Tanzania kuwa ya kidijitali kwa kuibadilisha nchi na utumishi wa umma kupitia sera na mbinu mbalimbali za utendaji kazi serikalini ili kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kutumia TEHAMA.

Bw. Xavier ameongeza kuwa, kukutana kwa wadau mbalimbali katika kikao kazi hicho kutoka katika Wizara, Taasisi na Mashirika iwasaidie kujadili hali ya utekelezaji wa serikali mtandao katika taasisi za umma zikiwemo changamoto na mbinu za kukabiliana nazo ili kupunguza gharama za uendeshaji wa serikali.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mhandisi Benedict Ndomba amesema kuwa, miradi ya mifumo ya TEHAMA katika taasisi za umma nchini kupitia kaulimbiu ya kikao kazi hicho ikizingatia Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo ya Serikali Mtandao katika ujenzi wa miundombinu na mifumo ya TEHAMA itasaidia kupunguza urudufu wa mifumo, kurahisisha taasisi za umma kubadilishana taarifa na kuokoa fedha za umma kwa kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali.

Kikao kazi hicho kilichoanza tarehe 06 Februari, 2024 na kuhitimishwa leo tarehe 08 kimebeba kaulimbiu ya “Uzingatiwaji wa Sera, Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Ubadilishanaji salama wa Taarifa”.

 













Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na washiriki wa kikao kazi cha nne cha serikali mtandao wakati akifunga kikao kazi hicho jijini Arusha kilichoandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).


Washiriki wa kikao kazi cha nne cha serikali mtandao wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) wakati akifunga kikao kazi hicho jijini Arusha kilichoandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).




Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Xavier Daudi akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete kwa kufunga kikao kazi cha nne cha serikali mtandao jijini Arusha. 


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Mhandisi Benedict Ndomba akieleza lengo la kikao kazi cha nne cha serikali mtandao kabla ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete kukifunga kikao hicho jijini Arusha. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akisisitiza jambo kwa washiriki wa kikao kazi cha nne cha serikali mtandao wakati akifunga kikao kazi hicho jijini Arusha kilichoandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitazama kifaa cha kupima kiasi cha gesi na mafuta alipotembelea banda la Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wakati wa kikao kazi cha nne cha serikali mtandao kilichofanyika jijini Arusha.




Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitazama kipeperushi cha Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) alipotembelea banda hilo wakati wa kikao kazi cha nne cha serikali mtandao kilichoandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) jijini Arusha.




Tuesday, February 6, 2024

MHE. SIMBACHAWENE AWATAKA WATAALAM WA TEHAMA KUTATUA CHANGAMOTO WANAZOKUTANA NAZO WANANCHI WANAPOTUMIA MIFUMO YA TEHAMA

 Na. Veronica Mwafisi-Arusha

Tarehe 06 Februari, 2024

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewataka watalaam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutatua changamoto wanazokutana nazo wananchi wanaotumia mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo wakati akifungua kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

“Nina furaha kubwa kwamba leo ninazungumza na watu sahihi, hivyo ni imani yangu kuwa, kwa muda huu wa siku tatu mtakaokuwa hapa mtaweza kuzungumza yale yaliyofanikiwa katika TEHAMA, mtakubaliana kwa uwazi lakini pia mtazungumzia changamoto ambazo wateja wetu wanaotumia mifumo ya TEHAMA wanakutana nazo,” Mhe. Simbachawene amesisitiza. 

Ameongeza kuwa, kuimarika kwa Taasisi ya eGA kunatokana na nia ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukuza matumizi ya TEHAMA katika utendaji kazi wa Serikali ili kuwezesha utoaji wa huduma kwa umma kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa urahisi popote walipo.

Amesema pamoja na yote yatakayozungumzwa katika kikao kazi hicho, kikubwa ni suala la utoaji wa huduma kwa wananchi, kipimo chake ni dhahiri kwani wananchi wakilalamika na kukaa kwenye foleni maana yake watumishi hawajatimiza wajibu wao.

Hivyo kila mmoja awajibike katika eneo lake ili kufikia azma ya dhati ya Rais. Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya utoaji wa huduma bora kwa umma kwa ustawi wa taifa.

Akimkaribisha Waziri Simbachawene kufungua kikao kazi hicho, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amesema katika kuhakikisha TEHAMA inaimarika Serikalini kama ambavyo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mara kwa mara, Ofisi ya Rais-UTUMISHI itaendelea kuboresha miundo ya kiutumishi pamoja na stahiki za wataalam wa TEHAMA ili kuhakikisha wanatumia taaluma zao ipasavyo kuleta matokeo chanya kwa maendeleo ya taifa letu.

Amesema mafanikio ya Serikali Mtandao ni jumuishi kwa kada zote hivyo Ofisi ya Rais-UTUMISHI itaendelea kusimamia na kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kada zote ili kufanikisha ujenzi wa Serikali ya Kidijitali.

Akielezea majukumu ya utekelezaji wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mkurugenzi Mkuu wa eGA Mhandisi Benedict Ndomba amesema Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na dhamira yake ya dhati ya kutaka kuwa na Serikali Mtandao, kupitia Ofisi ya Rais-UTUMISHI amekuwa akitenga fedha za kutosha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya TEHAMA.

Amesema zaidi ya washiriki 1,000 kutoka taasisi za umma wanashiriki kikao kazi hicho kinaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Uzingatiwaji wa Sera, Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao Kwa Ubadilishanaji Salama wa Taarifa.’

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akifungua kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Sehemu ya washiriki wa kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati akifungua kikao kazi hicho katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi, akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Mhandisi Benedict Ndomba akielezea majukumu ya eGA kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akifuatilia kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).