Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maadali, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Felister Shuli, Leo Septemba 4, 2026 katika Ukumbi wa Sekretariet ya Ajira ameongoza mafunzo ya maadili kwa wanamichezo wa Ofisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha wanamichezo wanaoshiriki mashindano kuzingatia misingi ya uadilifu, nidhamu, heshima na weledi.
Mafunzo hayo yamejikita katika kuwaelimisha wanamichezo kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma, sheria, taratibu na kanuni zinazoongoza utendaji wa mtumishi wa umma wakati wa mashindano ya SHIMIWI 2026 na Mengine.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Shuli amewataka wanamichezo hao kutambua kuwa wanaposhiriki katika mashindano, wanabeba taswira ya Ofisi ya Rais – Utumishi na hivyo wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika nidhamu, mwenendo na matumizi sahihi ya lugha na vitendo.
“Mnapokuwa uwanjani, siyo tu mnashindana kama wanamichezo, bali pia mnawakilisha taasisi yenu na Utumishi wa Umma kwa ujumla. Hivyo, kila mmoja anapaswa kuhakikisha mwenendo wake unaendelea kulinda heshima na taswira ya Ofisi,” amesisitiza.
Aidha, amewahimiza wanamichezo hao kutumia mafunzo hayo kama sehemu ya kujijenga katika maisha ya kila siku, kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji, kuheshimu viongozi, waamuzi, wapinzani na wenzao, pamoja na kuepuka vitendo vinavyoweza kuathiri taswira ya taasisi.
Kwa upande wao, wanamichezo walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maadili, nidhamu na wajibu wao kama watumishi wa umma wanaoshiriki michezo.
Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Ofisi ya Rais – Utumishi katika kuimarisha uelewa wa watumishi kuhusu maadili ya Utumishi wa Umma, huku michezo ikiendelea kutumika kama nyenzo ya kujenga afya, mshikamano, ushirikiano na kuongeza tija mahali pa kazi.









No comments:
Post a Comment