Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha taaluma na kazi ya Udereva nchini kwa lengo la kuhakikisha inakuwa na staha, hadhi na heshima sawa na kada nyingine katika Utumishi wa Umma.
Akijibu Swali Na. 59 lililoulizwa Bungeni jijini Dodoma na Mbunge wa Mlalo, Mhe. Rashid Abdallah Shangazi, kuhusu mkakati wa Serikali wa kuhakikisha taaluma na kazi ya udereva inakuwa na staha, hadhi na heshima, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Regina Qwaray amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kimkakati katika eneo hilo.
Amesema miongoni mwa hatua hizo ni kuboresha Muundo wa Maendeleo ya Utumishi wa Kada ya Udereva, hatua inayolenga kuimarisha nafasi na maendeleo ya watumishi katika kada hiyo pamoja na kuweka mazingira yanayowezesha utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi.
“Serikali imeendelea kuboresha mafunzo ya kitaaluma na viwango vya elimu kwa kada ya udereva ili kuwawezesha watumishi kuwa na ujuzi na weledi unaoendana na mahitaji ya sasa ya utendaji kazi” amesema Qwaray.
Aidha, amesema Serikali pia inaendelea kuimarisha motisha na maslahi ya kada ya udereva, hatua ambayo inalenga kuongeza morali, ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesisitiza kuwa hatua hizo zinaendelea kuzingatia umuhimu wa kuhakikisha kada ya udereva inakuwa na mazingira bora ya utendaji kazi yanayomwezesha mtumishi kukidhi na kumudu mazingira ya utendaji kazi na hivyo kuchangia katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

No comments:
Post a Comment