Wednesday, September 9, 2026

OR – UTUMISHI, UNESCO KUANDAA PROGRAMU MAALUM YA KUWAJENGEA UWEZO WATUMISHI MATUMIZI YA AKILI UNDE

 Na Eric Amani, Dodoma

Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala na Utawala Bora kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), imeandaa programu maalum ya kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma kuhusu matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI)

Hayo yamebainishwa leo Septemba 9, 2026 Mtumba jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais -UTUMISHI, Bi. Leila Mavika wakati wa kikao kazi na wadau wa UNESCO katika kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Amesema programu hiyo inalenga kuongeza uelewa na ujuzi wa Watumishi wa Umma kuhusu matumizi sahihi na yenye tija ya Akili Unde katika mazingira ya kazi, pamoja na kuwawezesha kutumia teknolojia hiyo katika kuongeza ufanisi, ubunifu na tija katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Bi. Mavika amesema programu hiyo inatekelezwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo na maazimio yaliyotokana na Mkutano wa UNESCO wa mwaka 2025 kuhusu masuala ya elimu ya Akili Unde na mabadiliko ya kidijitali.

Amesema maendeleo ya teknolojia hiyo yanatoa fursa kwa Taasisi za Serikali kurahisisha mchakato wa kiutendaji, kuimarisha uchambuzi wa taarifa na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Matumizi ya Akili Unde yanapaswa kuzingatia usalama wa taarifa, faragha, maadili, Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma,” amesema Bi. Mavika.

Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais–UTUMISHI na UNESCO unalenga kujenga Watumishi wa Umma wenye ujuzi na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia na kutumia Akili Unde kwa uwajibikaji.

Programu hiyo inatarajiwa kuongeza tija na ufanisi katika Utumishi wa Umma na kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais -UTUMISHI, Bi. Leila Mavika wakati wa kikao kazi na wadau wa UNESCO katika kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi Leo Septemba 9, 2026

Mkuu wa Habari na Mawasiliano shirika la UNESCO Bi. Nancy Angulo akimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais -UTUMISHI, Bi. Leila Mavika (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi Leo Septemba 9, 2026 katika Ofisi hiyo iliyopo Mtumba Dodoma


Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais -UTUMISHI, Bi. Leila Mavika (Kulia) akimsikiliza Bi. Nancy Angulo (Kushoto) wakati akizingumza kwenye kikao kazi kilichofanyika katika ofisi ya Rais – UTUMISHI Leo Septemba 9, 2026



Mkurugenzi wa Tehama Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Priscus Kiwango akimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais -UTUMISHI, Bi. Leila Mavika (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi Mtumba Dodoma

Mkurugenzi wa Mawasiliano Serikalini Bi. Mary Mwakapenda akimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais -UTUMISHI, Bi. Leila Mavika (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi Mtumba Dodoma.

Picha ya pamoja ya Kaimu Katibu Mkuu Bi Leila Mavika (Katikati) na baadhi ya viongozi kutokea shirika la UNESCO na Wizara ya Mawasiliano leo Septemba 9, 2026




No comments:

Post a Comment