Thursday, September 3, 2026

TIMU YA MPIRA WA PETE UTUMISHI YAENDELEA KUIMARIKA, YAICHAPA DOM KINGS 68–42

 Na Eric Amani, Dodoma

Timu ya Mpira wa Pete ya Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeendelea kuonyesha kiwango kizuri na kuimarika kuelekea mashindano ya SHIMIWI 2026, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 68–42 dhidi ya timu ya Dom Kings katika mchezo wa mazoezi uliofanyika Agosti 2, 2026 jijini Dodoma.

Katika mchezo huo, Utumishi ilionesha uwezo mzuri wa kiufundi, kasi, umakini na ushirikiano wa wachezaji, hali iliyoiwezesha kutawala mchezo na kupata ushindi wa mabao 68, huku Dom Kings ikiambulia mabao 42.

Mchezo huo ni sehemu ya maandalizi ya timu hiyo kuelekea Mashindano ya Michezo ya Wizara, Idara za Serikali na Mikoa (SHIMIWI) 2026, yanayotarajiwa kufanyika mkoani Kilimanjaro. Maandalizi ya mashindano hayo yameendelea kushika kasi, huku taasisi mbalimbali za Serikali zikiendelea kuimarisha timu zao kupitia mazoezi na michezo ya kirafiki.

Ushindi dhidi ya Dom Kings unaongeza morali kwa kikosi cha Utumishi na kutoa fursa kwa benchi la ufundi kuendelea kutathmini uwezo wa wachezaji, kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kujenga muunganiko bora wa timu kabla ya kuingia kwenye ushindani wa SHIMIWI 2026.

Kwa upande wa wachezaji, ushindi huo umeonesha dhamira yao ya kufanya vizuri katika mashindano hayo, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendelea na mazoezi, nidhamu na mshikamano ili kuhakikisha timu inakuwa tayari kwa ushindani mkubwa.









No comments:

Post a Comment