Na Lusungu Helela, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka watumishi wa umma kuhakikisha wananchi wanapata huduma za Serikali popote walipo kwa kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), badala ya kulazimika kusafiri hadi Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Rais Mhe. Samia ametoa agizo hilo leo, Ijumaa Oktoba 30, 2026, wakati wa uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba, ambapo akiwa na Rais wa Jamhuri ya Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço, amekata utepe katika jengo la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kuashiria ufunguzi wa majengo yote ya ofisi za wizara na taasisi za Serikali yaliyojengwa katika mji huo.
Amesema kukamilika kwa majengo hayo hakumaanishi wananchi wote wanapaswa kusafiri hadi Mtumba kupata huduma, bali taasisi za Serikali zinapaswa kutumia mifumo ya TEHAMA kurahisisha utoaji wa huduma katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesisitiza umuhimu wa mifumo ya TEHAMA inayotumiwa na taasisi za Serikali kuweza kubadilishana taarifa ili kuwaondolea wananchi usumbufu wa kuwasilisha taarifa zilezile katika ofisi tofauti.
"Mwananchi hatakiwi kupeleka taarifa ileile aliyopeleka katika moja ya ofisi za Serikali. Ndiyo maana mara nyingi nimekuwa nikisisitiza mifumo ya TEHAMA ni lazima isomane ili kuwaondolea usumbufu wananchi wanapohitaji huduma katika ofisi za Serikali," amesema Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumzia jengo la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambalo limetumika kuashiria ufunguzi wa majengo yote ya Serikali Mtumba, Rais Samia amesema amepata fursa ya kutembelea ndani ya jengo hilo na kujionea mifumo ya TEHAMA iliyowekwa kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ameeleza matumaini yake kuwa majengo mengine ya wizara na taasisi za Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba pia yamewekewa mifumo inayowezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi.
Aidha, amewataka watumishi wa umma kuyatunza majengo ya Serikali yaliyojengwa Mtumba ili yadumu na kuendelea kutumika kwa manufaa ya wananchi.
Uzinduzi huo umehusisha pia barabara za Mji wa Serikali Mtumba, ikiwa ni sehemu ya shughuli zilizofanyika katika hafla hiyo jijini Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.
Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake
Rais wa Jamhuri ya Angola, Mhe. João Manuel Conçalves Lourenço wakimsikiliza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati akitoa maelezo kuhusiana na jengo la Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora mara baada ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan
na mgeni wake wakiwa pamoja na viongozi
wengine kukata utepe kuashiria ufunguzi wa majengo yote ya ofisi za wizara na
taasisi katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma, tarehe 30 Oktoba, 2026.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa pamoja na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Angola, Mhe. João Manuel Conçalves Lourenço, kuashiria ufunguzi wa majengo yote ya ofisi za wizara na taasisi katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma, tarehe 30 Oktoba, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. SamiaSuluhu Hassan, akikata utepe pamoja na mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Angola Mhe. João Manuel Conçalves Lourenço kuashiria ufunguzi wa barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma, tarehe 30 Oktoba, 2026.



No comments:
Post a Comment