Na. Antonia Mbwambo – Dodoma
Tarehe 9
Oktoba, 2026
Kaimu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Bw. Cyrus Kapinga, amewahimiza wananchi na Watumishi wa Umma wanaopata huduma
kwa njia ya mtandao na wale wanaotembelea Ofisi hiyo kuendelea kutoa maoni na
mapendekezo yatakayochangia kuboresha huduma zinazotolewa.
Bw.
Kapinga ametoa wito huo Oktoba 9, 2026, wakati akimwakilisha Katibu
Mkuu-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi, katika hafla ya kilele cha Wiki ya Huduma kwa
Mteja iliyofanyika katika eneo maalumu la Ofisi hiyo, Mtumba, jijini Dodoma.
Amesema
maoni na mrejesho kutoka kwa wateja ni nyenzo muhimu katika kutathmini ubora wa
huduma, kutambua changamoto na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho ili
kuongeza ufanisi na kukidhi mahitaji ya wananchi na Watumishi wa Umma.
“Tunawahimiza
wananchi na Watumishi wa Umma kupitia mtandao na wale wanaotembelea Ofisi yetu
kupata huduma mbalimbali kuendelea kutoa maoni na mapendekezo kwani mrejesho
wao utatusaidia kutambua mapungufu na maeneo yanayohitaji maboresho ili
kuimarisha utoaji wa huduma,” amesema Kapinga.
Aidha, Bw. Kapinga ameeleza kuwa Ofisi hiyo
imeweka utaratibu wa kupokea maoni na mrejesho kutoka kwa wateja kupitia njia
mbalimbali, zikiwemo sanduku la maoni, mitandao ya kijamii, simu ya huduma kwa
wateja na mfumo wa e-Mrejesho. Amewahimiza wananchi na Watumishi wa Umma
kutumia njia hizo kuwasilisha maoni, ushauri na mapendekezo yao kwa lengo la
kuboresha huduma zinazotolewa.
Bw.
Kapinga amewashukuru wananchi na Watumishi wa Umma wanaoendelea kutumia huduma
za Ofisi hiyo, huku akiwakaribisha kuendelea kunufaika na huduma hizo kwa
maslahi ya Taifa.
No comments:
Post a Comment