Waamini wa Kanisa katoliki wameaswa kuwalea na kuwatunza mapadri kwa kuwa mapdri hao wametoa maisha yao kwa Mungu ili kuwasaidia watu kuishi maisha ya utimilifu wa kiroho kwa kuwaongoza kupitia maandiko na kufikia ufalme wa Mbingu.
Tafakari hiyo imetolewa leo Agosti 22, 2024 na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
George Simbachawene wakati alipokuwa akiongea na waamini wa Jimbo la Mbulu
wakati wa Jubilei ya Miaka 25 ya Upadri wa Mha. Askofu Antony Lagwen iliyofanyika
jimboni humo.
Alisema kuwa kila muamini kwa nafasi yake anatakaiwa
kujitafakari kama anatimiza wajibu wake sawa sawa kwa Mungu ikiwa ni pamoja na
kujitolea kuwalea hao wanaowaita ‘Baba’
kwa kuwa wamekwisha jitoa sadaka kwa
ajili ya kuukomboa ulimwengu.
“Waminini wenzangu, tunatakiwa kuwalea hawa tunaowaita
‘Baba’ ‘Baba’
ambao ni maaskofu na mapadri, hao ni binadamu na wanamahitaji muhimu kama sisi mathalani
chakula, nguo, matibabu, usafiri na nyumba za kuishi, hivyo nguvu tunazoweka
katika ujenzi wa makanisa ni sawa, kutoa sadaka ni sawa, kutoa zaka ni sawa.
Kwa umoja huo huo tushiriki kutimiza mahitaji yao ya kimwili ili hata ya kiroho
yaweze kwenda vyema” alisisitiza Mhe. Simbachawene.
Aidha, aliongeza kuwa ni wajibu wa waamini kutambua
kuwa wazazi wa mapadri hawa walitoa watoto wao sadaka kwa Mungu na hivyo ni
wajibu wa kanisa ambao ni waamini wote kushirikiana katika kuwalea na kuwatunza
kwa hali na mali.
Vilevile, Mhe. Simbachawene amemuomba Mha. Askofu
Antony G. Lagwen kupokea salaam za pongezi kutoka kwa Rais Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan na ameahidi kuendelea kushirikiana na kanisa Katoliki katika
Nyanja mbalimbali ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
Awali, Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Arusha Mha.
Josaphat Lebulu katika Mahubiri yake amewasisitiza mapadri kutokuwazuia waamini
kufanyia Jubilee kwa kuwa Upadri ni zawadi ya Mungu katika nafasi zao.
“Tunatakiwa kuwa kitu kimoja na Mungu na Mungu anakuwa
kitu kimoja na sisi, hivyo tuukanyage kabisa uovu na tuushinde uovu kwa wema” aliongeza Mha. Lebulu
Vilevile, katika Salaam za shukrani Askofu wa Jimbo
Katoliki la Mbulu Mha. Antony Gaspar Lagwen ambaye ameazimisha Jubilee ya miaka
25 (1999-2024) ya Upadri, aliishukuru
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kushirikiana na Kanisa na kuhakikisha
kunakuwa na maendeleo kwa wananchi.
Mha. Lagwen ameiomba Serikali kuendelea kuwa karibu na
Kanisa Katoliki sio tu kwa maendeleo ya
Kanisa bali ili jamii ipate huduma na kujijenga inavyopasa katika masuala ya
uboreshaji wa mazingira, utawala bora na kulinda utu wa mtu wakati wote kwa
ustawi wa taifa.
No comments:
Post a Comment