“Ninamuelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, kushirikiana na Katibu Mkuu TAMISEMI ili kuhakikisha shule zote mpya na vituo vya afya nchi nzima vilivyokamilika vinapangiwa Walimu na Madaktari mtawalia”.
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la
Kibakwe Mhe. George Simbachawene Agosti 7, 2024 wakati alipokuwa akiongea na
wananchi wa Kata ya Wangi Jimbo la Kibakwe kwenye mkutano wa hadhara alipokuwa
akiongea na wananchi na kuzindua Shule ya Sekondari Wangi.
“Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ajira zaidi
ya elfu 12 kwa sekta ya afya na nyingine kwa sekta ya elimu, hivyo hatuna budi
kuhakikisha wanapangwa vizuri ili wananchi wapate huduma ipasavyo” alisema Mhe. Simbachawene.
Aidha, Mhe. Simbachawene amewaomba wananchi wa Kata ya
Wangi na Wotta kushukuru kwa maendeleo ambayo yameletwa na Rais Dkt. Samia mathalani
ujenzi barabara, shule na vituo vya afya kwa lengo la kurahisisha maisha kwa
Wananchi.
Hivyo, wananchi wameombwa katika uchaguzi mkuu wa
mwaka 2025 kumpa kura za ndiyo Rais Mhe. Dkt. Samia, Mbunge Mhe. Simbachawene
na Madiwani ili waenedelee kutekeleza maono waliyonayo badala ya kuanza upyya.
Mhe. Simbachawene anaendelea na ziara yake katika Jimbo
la Kibakwe ambapo amefanya mikutano ya hadhara katika Kijiji cha Wotta na Wangi
Jimbo la Kibakwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.
No comments:
Post a Comment