Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe Mhe. George Simbachawene ameelekeza viongozi wa maji katika kata ya Chipogolo Jimbo la Kibakwe kuuza maji kwa shilingi elfu moja mia mbili tu ili wananchi wengi waweze kumudu gharama na kuyatumia maji ipasavyo.
Maelekezo hayo yametolewa na Mhe. Simbachawene wakati
alipokuwa akiongea na wananchi wa Chipogolo kwenye mkutano wa hadhara uliolenga
kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
“Nimesikia kilio chenu kuhusu gharama kubwa za maji na
inaonekana ni kero kubwa. Sasa niwahakikishie kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan anawapenda sana na hataki kusikia wananchi wake wanapata shida ya huduma
yoyote. Hivyo, ninawaelekeza viongozi wanaosimamia huduma ya maji hapa
Chipogolo kuacha kuwatoza wananchi kiasi cha shilingi elfu mbili kwa unit isipokuwa kuanzia kesho tarehe 3 Agosti, 2024 itakuwa ni Shilingi elfu
moja na mia mbili tu” alisema Mhe. Simbachawene.
Aidha, Mhe. Simbachawene amewaomba wananchi wa
Chipogolo kufumbua macho, kutazama na kushukuru kwa maendeleo ambayo yameletwa
na Rais Dkt. Samia kwa kuwa barabara sasa ni nzuri, zahati, maji yapo, ujenzi
wa shule unaendelea na huduma nyingine nyingi zinaendelea kutekelezwa.
Hivyo, wananchi wameombwa katika uchaguzi mkuu wa
mwaka 2025 kumpa kura zote za ndiyo Rais Mhe. Dkt. Samia, Mbunge Mhe. Simbachawene
na Madiwani ili waenedelee kuijenga nchi kwa kasi.
Mhe. Simbachawene anaendelea na ziara yake katika Jimbo la Kibakwe ambapo amefanya mikutano ya hadhara katika Kijiji cha Muungano, Wiyenzele na Chipogolo katika kata ya Chipogolo, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.
No comments:
Post a Comment