Na. Mwandishi wetu
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Mhe. Deus Sangu ametoa rai kwa watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuwa wabunifu ili fedha zinazopelekwa kwa wananchi zisiende kama msaada
isipokuwa ziende kwa mantiki ya kuwainua na kuwatoa kwenye wimbi la umaskini.
Mhe. Sangu ametoa rai hiyo leo tarehe 19 Agosti, 2024 jijini Dar es
salaam wakati alipofanya ziara ya kujifunza namna taasisi hiyo inavyofanya kazi
na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi.
Amesema, mpango wa kunusuru kaya maskini ni muhimu sana kwa wananchi, hivyo alielekeza menejimenti kuendelea
kufikiri na kufungamanisha programu za kunusuru kaya maskini na programu
nyingine ili kuwatoa walengwa kwenye umaskini.
Aidha, aliongeza kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kutafuta
fedha na kuzipeleka kwa walengwa wengi zaidi, hivyo jitihada za kunusuru kaya
maskini zinatakiwa kuimarishwa zaidi na watendaji.
Aidha, Mhe.
Sangu ameomba menejimenti
na watumishi wa TASAF kumpa ushirikiano hasa anapotaka taarifa za mfuko ili kujibu hoja na kutoa ufafanuzi wa
masuala mbalimbali ya TASAF kwa Waheshimiwa Wabunge.
“Mimi milango iko wazi wakati wote, iwapo mtapata changamoto yoyote
inayohitaji mawazo au ushauri wangu, niko tayari kuwasaidia kwa kuwa ni sehemu
ya utekelezaji wa majukumu yangu” alisisitiza Mhe. Sangu.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Shedrack Mziray alisema malipo
ya ruzuku kwa walengwa hufanywa kwa kutoa fedha taslimu kwa kutumia kamati ya
usimamizi wa shughuli za mipango kwa jamii chini ya usimamizi wa ngazi ya
utekelezaji wa mpango (Halmashauri) na njia ya pili ni ya kieleketroni.
Bw. Mziray ameongeza kuwa njia zote ni muhimu kwa walengwa ingawa njia
ya kieletroni ni muhimu zaidi kwa kuwa inarahisisha utoaji wa ruzuku kwa walengwa
ingawa kuna changomoto mbalimbali zinazowakabili wanufaika.
Alibainisha kuwa mwaka 2023 TASAF ilifanya tathmini na kubaini kaya za walengwa 394,305 zimeimarika kiuchumi na kukidhi vigezo vya kuhitimu na hivyo hazitaendelea kupewa ruzuku kama ilivyokuwa hapo awali.
Mhe. Sangu amefanya ziara kwa lengo la kujifunza kuhusu majukumu ya Mfuko
huo ambao upo chini ya Ofisi anayoiongoza.
No comments:
Post a Comment