Friday, August 23, 2024

MHE. SANGU ATOA RAI KWA VIONGOZI WA UMMA

 Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu ametoa rai kwa Viongozi wa Umma kuwa waadilifu kwa kuwa wana dhamana ya kusimamia taasisi na kufanya maamuzi katika Utumishi wa Umma.

Mhe. Sangu ametoa rai hiyo leo Agosti 23, 2024 wakati alipofanya ziara katika ofisi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyopo katika jengo la Maadili (Maadili House) Jijini Dodoma kwa lengo la kujifunza majukumu yanayotekelezwa na taasisi hiyo.

“Hakikisheni mnatumia Sheria, Miongozo na Kanuni katika kusimamia maadili ya Viongozi katika Utumishi wa Umma, maadili ndio kila kitu, iwapo hatutaweka msingi wa maadili vizuri utoaji wa huduma Serikalini hautokuwa na tija na malalamiko ya wananchi hayawezi kukoma” amesisitiza Mhe. Sangu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona wananchi wanapata huduma vizuri lakini baadhi ya viongozi wa umma wanashindwa kuzingatia maadili katika utoaji wa huduma, hivyo kuathiri nia njema ya Rais.

Aidha amebainisha kuwa, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni taasisi muhimu sana kwa kuwa chimbuko lake ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977. Hivyo, wanatakiwa kufanya kazi kwa kiwango cha hali ya juu wakizingatia kwamba ni taasisi tegemewa kwa ustawi wa Taifa.

Aidha, amesema kuwa, Viongozi wa Umma wasipozingatia utalaam, uaminifu na kutimiza wajibu wao ipasavyo matokeo yake ni kuvunja Sheria, kuwa na mwenendo usioridhisha na kufanya matukio yenye athari na hasara kwa wananchi na taifa kwa jumla.

Awali, Kaimu Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Waziri  Kipacha amebainisha kuwa moja ya changamoto kubwa katika usimamizi ni kwa baadhi ya viongozi wa umma ambao wamebainika kujaza taarifa zisizo sahihi kwenye matamko ya rasilimali na madeni, hivyo wamebaini mbinu za kisasa katika kufanya uchunguzi wa masuala ya  kimaadili.

Aidha, amesema kuanzia Oktoba 2024, Viongozi wote watatakiwa  kutumia mfumo wa Online Declaration System (ODS) unaopatikana kupitia tovuti ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa ajili ya kujaza taarifa za Matamko ya Rasilimali na Madeni na kuziwasilisha kwa njia mtandao.

“Sisi kama Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Tutakupa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu uliyopewa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan” amesema Bw. Kipacha.

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ina Ofisi  Dodoma, Morogoro, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Tabora, Mtwara na Mbeya ambazo zinaendelea na majukumu yake ikiwemo kuchunguza mwenendo na tabia za viongozi wa utumishi wa umma.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akizungumza na viongozi na watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji jijini Dodoma.


Baadhi ya watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu alipokuwa akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi katika ofsi hiyo jijini Dodoma.



Kaimu Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma, Bw. Waziri Kipacha (Aliyesimama) akielezea utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji.


Mkurugenzi Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bi. Teddy Njau akitoa utambulisho wa viongozi na watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kabla ya kuanza kwa kikao cha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu.

Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu wakati akizungumza nao alipotembelea ofisi hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.


Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bi. Margaret Kahurananga akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu mara baada ya kuhitimisha ziara ya kikazi katika ofisi hiyo.



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu (katikati aliyekaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na watendaji wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi jijini Dodoma.

 












No comments:

Post a Comment