Friday, August 30, 2024

KAMATI YA BUNGE YATOA MAELEKEZO KWA TAKUKURU NA SEKRETARIETI YA AJIRA

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Florent Kyombo na Wajumbe wa Kamati hiyo wamezielekeza taasisi za TAKUKURU na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kufanya kazi kwa ufanisi ili kujenga imani kwa wananchi juu ya huduma wanazozitoa.

Mhe. Kyombo amesema hayo leo jijini Dodoma wakati wa semina kwa wajumbe wa kamati hiyo iliyotolewa na TAKUKURU kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma. Semina hiyo ililenga kuwajengea Wajumbe uelewa mpana ili waweze kufanya uamuzi wa masuala mabalimbali kwa maslahi mapana ya nchi.

Mhe. Kyombo ameielekeza Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna mchakato wa ajira unavyofanyika ili kuondoa dhana ya wananchi kuwa nafasi za kazi ni kwa ajili ya kundi fulani.

"Wananchi wote wanahaki ya kuomba nafasi ya kulitumikia taifa lao kwa kuomba Ajira Serikalini kupitia Sekretarieti hii, hivyo waelimisheni kuwa mchakato ni wazi kwa yeyote mwenye sifa na akishinda anapata nafasi" alisisitiza Mhe. Kyombo.

Kadhalika Mhe. Kyombo ameipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kuwa na watumishi waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mhe. Kyombo ametoa wito kwa taasisi hiyo kujikita zaidi katika kuongeza rasilimali fedha na vitendea kazi ili kutoa mchango wenye tija katika kufanya kazi na kufikia lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora kupitia taasisi hizo na taasisi nyingine zilizo chini ya ofisi hiyo zitafanya kazi kwa weledi na ufanisi.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Chonga Pemba (ACT), Mhe. Salum Shaafi amezishukuru taasisi hizo kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamepanua uelewa wap kuhusu majukumu ya taasisi hizo muhimu kwa taifa.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Florent Kyombo akizungumza wakati akifungua semina iliyotolewa na TAKUKURU na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa Wajumbe wa Kamati hiyo jijini Dodoma.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakifuatilia mada kutoka kwa Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma-TAKUKURU, Bw. Joseph Mwaiswelo (hayupo pichani) wakati wa semina iliyotolewa na Taasisi hiyo.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Florent Kyombo (hayupo pichani)  kuzungumza wakati wa semina iliyotolewa na TAKUKURU na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma jijini Dodoma.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakifuatilia mada iliyokuwa ikitolewa na Kaimu Katibu, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ambaye ni Mkuu wa Idara ya TEHAMA, Mhandisi Samwel Tanguye (hayupo pichani) wakati wa semina iliyotolewa na TAKUKURU na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma jijini Dodoma.



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akifuatilia mada kuhusu mwelekeo wa Serikali kwenye vita dhidi ya Rushwa. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Xavier Daudi.


Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila akielezea lengo kuu la semina inayotolewa na taasisi yake kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria iliyofanyika jijini Dodoma.



Kaimu Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ambaye ni Mkuu wa Idara ya TEHAMA, Mhandisi Samwel Tanguye akifanya wasilisho la mada kuhusu utekelezaji wa kibali cha ajira mpya kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria.


Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Xavier Daudi akijibu moja ya hoja iliyowasilishwa na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakati wa semina iliyotolewa TAKUKURU na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa Kamati hiyo jijini Dodoma. Wa kwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye


Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Seif Gulamali akiwasilisha hoja kwa Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma-TAKUKURU, Bw. Joseph Mwaiswelo (hayupo pichani) mara baada ya kuwasilisha mada kwenye semina kuhusu mwelekeo wa Serikali kwenye vita dhidi ya Rushwa.

Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Cyrus Kapinga (katikati) na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, SACP. Ibrahim Mahumi (wa kwanza kulia) wakifuatilia mada mbalimbali kwenye semina iliyotolewa na TAKUKURU na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma jijini Dodoma. Wa kwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye.

Baadhi ya Watumishi wa TAKUKURU wakiwa katika semina iliyotolewa kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa umma iliyofanyika jijini Dodoma.

























No comments:

Post a Comment