Na. Veronica Mwafisi-Bagamoyo
Tarehe 15 Julai, 2023
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Maafisa Utumishi wote kuhakikisha maombi yote ya watumishi wa umma nchini wanaostahili kupanda madaraja yanawasilishwa katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili yaweze kushughulikiwa kwa wakati kwa lengo la kutenda haki na kuondoa malalamiko yasiyokuwa na ulazima.
Mhe. Kikwete amesema hayo
alipokuwa akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo,
Mkoa wa Pwani wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji
na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.
“Serikali imeshatoa
maelekezo ya kuwasilisha maombi ya watumishi wa umma wanaostahili kupanda madaraja
ili yafanyiwe kazi, hivyo Afisa Utumishi hakikisha unahakiki vizuri na
kuwasilisha maombi ya kupandishwa madaraja kwa watumishi hawa,” amesisitiza Mhe.
Kikwete.
Mhe. Kikwete amesema
kuwa, Serikali inayoongozwa na Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan haina tatizo katika suala la kutafuta mafungu ya fedha kwa ajili ya
kuwapa watumishi wake stahili zao ili waweze kufanya kazi vizuri.
Mhe. Kikwete amesema
kuwa, Mhe. Rais Dkt. Samia anataka watumishi wake wawe na ari ya kufanya kazi
kwani kukiwepo na manung’uniko itaondoa morali ya kufanya kazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
wa Halmashauri ya
Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Shauri Selenda, amemshukuru Naibu Waziri Kikwete kwa kuhimiza
uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kusikiliza changamoto zinazowakabili
watumishi hao kwa ajili ya kuzifanyia kazi.
Aidha, Mkurugenzi Selenda amemshukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuendelea kutoa stahiki mbalimbali za watumishi ikiwemo upandishwaji vyeo,
ubadilishwaji kada, ajira mpya, vibali vya uteuzi, ulipaji wa malimbikizo ya
mishahara, fedha za matibabu, mafao ya uzazi, fidia za watumishi wanaoumia
kazini, pamoja na kuboresha vitendea kazi na maeneo ya kazi.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya
watumishi wengine, Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bw. George
Mwalukasa ametoa ahadi kwa Mhe. Naibu Waziri Kikwete kuwa watatekeleza
maelekezo yote ambayo amewaagiza na kuhakikisha kwamba watumishi wote waliokuwa
na changamoto za madaraja wanapatiwa ufumbuzi kama Serikali ilivyoelekeza.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani
Kikwete amehitimisha ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Pwani iliyokuwa na
lengo ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma,
kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma pamoja na kukagua
utekelezaji wa Miradi ya TASAF.
Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete
akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo,
Mkoa wa Pwani wakati wa ziara yake ya kikazi katika mkoa huo iliyolenga
kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.
Sehemu ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani wakimsikiliza
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa
ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi wa halmashauri hiyo.
Mbunge wa jimbo la Bagamoyo,
Mhe. Muharami Mkenge akitoa
salamu za wananchi na watumishi wa jimbo la Bagamoyo kwa Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) wakati wa ziara ya
kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua
changamoto zinazowakabili watumishi hao.
Mtumishi wa halmashauri
ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani Mwalimu Belloh Mkwazu (Aliyesimma)
akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu
Waziri huyo mkoa wa Pwani iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi hao.
Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (katikati) akisikiliza
hoja iliyokuwa ikiwasilishwa kwake na Mtumishi wa halmashauri ya Wilaya ya
Bagamoyo wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo mkoa wa Pwani iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi hao.
Afisa Utumishi wa
halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani Bw. George Mwalukasa akitoa
neno la shukrani kwa Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) mara baada ya Naibu Waziri huyo kuhitimisha
kikao kazi chake na watumishi wa halmashauri hiyo kilicholenga kuhimiza
uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.
No comments:
Post a Comment