Saturday, July 15, 2023

WAZIRI SIMBACHAWENE AWATAKA VIONGOZI KUSIKILIZA MALALAMIKO YA WATUMISHI

 Na. Lusungu Helela-Mpwapwa

Tarehe 15 Julai, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka viongozi wa ngazi za Wilaya na Halmashauri zote nchini kujenga utamaduni wa kusikiliza na kufanyia kazi malalamiko mbalimbali ya Watumishi wa Umma  huku akisema kiu yake ni kuona watumishi  hao wakifurahia kuwa Watumishi wa Wananchi. 

Waziri Simbachawene ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya  Mpwapwa mkoani Dodoma, ambapo amesema yeye kama kiongozi anatambua watumishi wanakabiliwa na changamoto lukuki na hawana sehemu ya kusemea. 

Amesema watumishi waliokata tamaa hawawezi kutoa huduma bora kwa wananchi huku akisisitiza kuwa hali hiyo imekuwa ikiwaumiza wananchi na kuifanya serikali iliyopo madarakani kuchukiwa kwa matatizo yao kutopatiwa ufumbuzi.

Amefafanua kuwa anataka kuona watumishi wa umma wakipata stahiki zao lakini na wao wakitekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Simbachawene amewataka Makatibu Tawala wa Wilaya nchini ambao ndio wakuu wa utumishi wa umma katika ngazi ya wilaya kutekeleza majukumu yao kwa kusikiliza vilio na malalamiko ya watumishi walio chini yao. 

"Watumishi waliochukia na wenye malalamiko hawawezi kuleta matokeo chanya ambayo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anakusudia, hivyo Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri na Katibu Tawala wa Wilaya shughulikieni matatizo ya watumishi" amesisitiza Mhe. Simbachwene.

Aidha, Mhe. Simbachawene amesema  Watumishi wa Umma wanaokiuka misingi ya utumishi wa umma akitolea mfano ulevi kazini ni vizuri wakawa wanaonywa kabla ya kuadhibiwa ikizingatiwa sasa hivi waajiriwa wengi ni vijana sana hivyo wanachohitaji ni malezi pekee.

Katika zoezi hilo la kusikiliza malalamiko ya watumishi, miongini mwa malalamiko yaliyotewa kwa wingi na watumishi hao ni kuchelewa kulipwa malimbikizo yao ya mishahara, kupandishwa madaraja, kuchelewa kulipwa fedha za uhamisho pamoja na kubambikiwa mikopo. 

Naye Mkuu wa wilaya ya Mpwapwa, Mhe. Sophia Kizigo amesema yeye na timu yake chini ya Katibu Tawala wa Wilaya watajipanga kusikiliza malalamiko ya watumishi ili kuhakikisha watumishi wa Mpwapwa wanaifurahia kazi yao.

Hata hivyo, Mhe. Kizigo ametumia fursa hiyo kuwaasa Watumishi wa Umma kuacha kukopea mshahara wote hali inayoufanya utumishi wa umma kudharauliwa kupelekea mtumishi kuishi maisha magumu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.


Sehemu ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa halmashauri hiyo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Bi. Mwanahamsi Ally Mara baada ya kuwasili katika halmashauri hiyo kwa ziara ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa halmashauri hiyo. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Mhe. Sophia Kizigo.



No comments:

Post a Comment