Thursday, July 13, 2023

WAZIRI SIMBACHAWENE AITAKA TASAF KUWA SHIRIKISHI ILI KUWAGUSA WALENGWA HALISI WA UMASIKINI

Na. Lusungu Helela-Dar es Salaam

Tarehe 13 Julai, 2023 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George ameutaka Uongozi wa  Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF)  kuwa shirikishi  katika mchakato wa kuwabaini walengwa halisi ambao ni maskini huku akiwasisitiza kuwatumia  Maafisa Maendeleo ya Jamii katika mchakato huo. 

Imeelezwa kuwa licha ya TASAF kufanya kazi yake nzuri ya kukwamua kaya masikini kwenye lindi la umasikini lakini kumekuwa na minong'ono kuwa wanaopata ruzuku hiyo sio walengwa halisi.

Kauli hiyo ameitoa leo Alhamisi Julai 13, 2023  wakati wa ziara yake ya kikazi  Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni muendelezo wa kuzungumza na Watumishi kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema Maafisa Maendeleo hao wa Jamii ni watu muhimu sana katika zoezi hilo  kwa vile wapo katika ngazi ya Kata  pamoja na ngazi ya Kijiji, hivyo wanawajua walengwa halisi. 

‘’Watumieni hawa kwani licha ya kuishi na walengwa hawa lakini pia Maafisa hawa wamekuwa wakishiriki katika vikao vya Madiwani’ amesisitiza Mhe Simbachawene.

Amefafanua kuwa, TASAF msingi wake ni  mpango shirikishi wa kuondoa umasikini hivyo, inatakiwa kuwashirikisha viongozi katika maeneo husika ili iweze kutimiza azma ya kuanzishwa kwake. 

Hata hivyo, Mhe.Simbachawene amesema TASAF bado inahitajika sana kwa vile bila uwepo wake, umaskini ungekuwa umeongezeka kwa kiasi kikubwa sana na kusisitiza kuwa itaendelea kuzikwamua kaya zilizoko kwenye umasikini uliokithiri.

Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Memejimenti ya Utumishi wa Umma, Mhe.Ridhiwani Kikwete amewapongeza watumishi wa TASAF kwa kazi nzuri wanayoifanya huku akisisitiza kuwa TASAF imesaidia ongezeko la wanawake katika shughuli za kiuchumi. 

Ameongeza kuwa kutokana na uwepo wa TASAF kumesaidia kupunguza migogoro kwenye ngazi ya kaya baada ya wananchi wengi maskini kujihusisha kwenye na uzalishaji mali.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Shedrack Mziray amesema atatekeleza maagizo yote yaliyotolewa na viongozi hao ikiwa ni  pamoja na kuhakikisha  walengwa wa ndio wanakuwa wanufaika namba moja.

TASAF ilianzishwa kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tatu lengo likiwa ni kuondoa umasikini uliokithiri kwa wananchi katika maeneo ya vijijini na maeneo machache ya mjini kwa kuwashirikisha kwenye shughuli za kiuchumi. 

1. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao. 

1.     Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuzungumza na watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi ya viongozi hao iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao. 


1.  Sehemu ya watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi jijini Dar es Salaam iliyolenga kuhimiza uwajibikaji. 


1.  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Bw. Shedrack Mziray akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa TASAF kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo jijini Dar es Salaam iliyolenga kuhimiza uwajibikaji.

1.  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiteta na Naibu Waziri wake, Mhe. Ridhiwani Kikwete kabla ya kuzungumza na watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi ya viongozi hao iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao. 

1.  Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akimuonyesha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene baadhi ya ofisi za TASAF wakati wa ziara ya kikazi ya viongozi hao iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa TASAF jijini Dar es Salaam.  

1.  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao. Wa pili kulia waliokaa ni Naibu Waziri wake, Mhe. Ridhiwani Kikwete na wa pili kushoto waliokaa ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Shedrack Mziray. 















No comments:

Post a Comment