Wednesday, July 12, 2023

NAIBU WAZIRI KIKWETE AWATAKA MAAFISA UTUMISHI KUWA WABUNIFU KATIKA UTENDAJI KAZI KWA MAENDELEO YA TAIFA

 Na. Veronica Mwafisi-Kisarawe

Tarehe 12 Julai, 2023

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Maafisa Utumishi nchini kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kuboresha utoaji wa huduma kwa  wananchi kwa maendeleo ya taifa.

Mhe. Kikwete amesema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa Umma Mkoa wa Pwani, Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi wa umma mkoani humo. 

“Nataka kusikia kila Afisa Utumishi anajiwekea ratiba ya kuzungumza na watumishi anaowasimamia ili kusikiliza maoni, malalamiko au changamoto zozote wanazokutana nazo kwa lengo la kuboresha utumishi wa umma nchini utakaoweza kuwahudumia wananchi kikamilifu,” amesema Mhe. Kikwete.

Aidha, Mhe. Kikwete amewataka Maafisa Utumishi kuweka utaratibu wa kujua mahitaji ya watumishi kwa kuzingatia hali halisi ili kukidhi haja mbalimbali za watumishi bila kuwa na malalamiko.

Mhe. Kikwete amesema kuwa, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka Maafisa Utumishi hao kuwa wasemaji wa watumishi wanaowasimamia na kutatua kero na changamoto zao.

Mhe. Kikwete amewasihi watumishi wa umma kuendelea kufanya kazi kwa juhudi, werevu na weledi mkubwa katika kuwatumikia wananchi

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Bw. Baptista Kihanza ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kupata rasilimaliwatu ambayo imesaidia kupunguza tataizo la uhaba wa watumishi katika halmashauri hiyo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete anaendelea na ziara ya kikazi katika Mkoa wa Pwani ikiwa leo ni siku ya tatu akilenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF katika mkoa huo ambapo leo alikuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.


Sehemu ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa halmashauri hiyo.


Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Wa kwanza kulia) akielekea kwenye ukumbi wa mikutano Mkoa wa Pwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kwa lengo la kuzungumza na watumishi wa halmashauri hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao. Katikati ni Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon.


Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Bw. Baptista Kihanza akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya halmashauri hiyo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi.




 

  

No comments:

Post a Comment