Na. Lusungu Helela-Dar es Salaam
Tarehe
14 Julai, 2023
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameitaka Taasisi ya UONGOZI (UONGOZI Institute) kufanya tafiti za kimkakati zitakazoweza kuibua masuala mbalimbali ya kiuongozi kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.
Waziri Simbachawene amesema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi ya UONGOZI jijini Dar es Salaam, ikiwa ni muendelezo wa kuzungumza na Watumishi kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema tafiti hizo zinatakiwa zilenge katika kuibua mijadala ambayo itachagiza dhana ya utawala bora kwa kujikita zaidi kuibua changamoto zinazosababishwa na viongozi wenyewe Barani Afrika.
"Tunataka mje na tafiti zitakazosomwa duniani kote ambazo zitaleta ukombozi kwa wananchi wa Bara la Afrika hususan katika masuala ya uongozi mfano kwenye suala la rushwa" amesema Mhe. Simbachawene.
Amefafanua kuwa kwenye masuala ya uongozi bado kunahitajika tafiti nyingi ambazo zitatoa dira ya kuwaandaa viongozi vijana wenye mtazamo wa kimapinduzi.
Katika hatua nyingine Mhe. Simbachawene ameipongeza Taasisi hiyo kwa kazi kubwa inayofanya ya kuwaandaa viongozi wa ndani na nje ya nchi pamoja kukutana na kuzungumza na viongozi mbalimbali.
"Ninajivunia kwa kazi zenu kwani huko nje taswira yenu ni kubwa mno na ya kimataifa kutokana na jitihada zenu mnazofanya za kuhakikisha Afrika inakuwa na viongozi wenye kuwahudumia wananchi " amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwan Kikwete ameihimiza Taasisi hiyo kuendelea kuandaa viongozi wa baadae watakaoweza kuendeleza mazuri yanayofanywa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Awali, Afisa
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo akiwasilisha taarifa ya
utekelezaji wa majukumu ya Taasisi yake, amesema atatekeleza maelekezo yote
yaliyotolewa ikiwa pamoja na kutoa tafiti zitakazoleta matokeo chanya katika
jamiii na taifa kwa ujumla.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na watumishi wa Taasisi
ya UONGOZI jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga
kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao. Katikati ni Naibu Waziri wake, Mhe.
Ridhiwan Kikwete na mwingine ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari
Singo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiangalia ofisi ya Taasisi
ya UONGOZI jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga
kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo. Aliombatana nao ni Naibu
Waziri wake, Mhe. Ridhiwani Kikwete na katikati ni Afisa Mtendaji Mkuu wa
Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari
Singo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa taasisi yake kwa Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George
Simbachawene wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo katika taasisi hiyo jijini
Dar es Salaam iliyolenga kuhimiza uwajibikaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja
na baadhi ya watumishi wa Taasisi ya UONGOZI jijini Dar es Salaam wakati wa
ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao. Wa pili
kulia waliokaa ni Naibu Waziri wake, Mhe. Ridhiwani Kikwete na wa pili kushoto
waliokaa ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo.
No comments:
Post a Comment