Tuesday, July 11, 2023

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN : RUSHWA INAZIDHOOFISHA NCHI ZA AFRIKA

Na. Lusungu Helela-Arusha

Tarehe 11 Julai, 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema tatizo la rushwa Barani Afrika limekuwa likidhoofisha mifumo ya kitaasisi na kuathiri mipango na mikakati ya kujikomboa kiuchumi jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma maendeleo huku idadi ya watu maskini ikizidi kuongezeka. 

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumanne Julai 11, 2023 wakati wa hotuba yake aliyoitoa jijini Arusha kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika, ikiwa ni siku ya tatu ya Maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila mwaka Julai 11. 

Amesema janga la rushwa linahitaji mbinu za kimkakati za kupambana nalo kwani ni miongoni mwa makosa yanayovuka mipaka ya nchi, hivyo ushirikiano wa pamoja baina ya nchi za Afrika hauepukiki. 

Kufuatia hatua hiyo, Rais Samia amewasihi viongozi wa Bara la Afrika kuchukua hatua stahiki kwa wala rushwa wote ili kutuma ujumbe duniani kote kwamba nchi za Afrika sio vichaka vya kuficha fedha zilizotokana na rushwa. 

 "Tunataka dunia nzima ifahamu kuwa, Afrika sio salama kwa wala rushwa, na hilo lionekane kwa vitendo kupitia hatua tunazozichukua dhidi ya wala rushwa na sio mikutano, makongamano na maneno peke yake" amesisitiza Rais Samia.  

Aidha, Rais Samia ameongeza kuwa Maadhimisho yawe fursa muhimu kwa nchi za Afrika kujitafakari kwa kina, uwazi na kwa dhati kuhusu utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kuzuia na Kupambana Rushwa ili ziweze kupata mafanikio ya pamoja na kutafuta njia bora za kutatua changamoto hizo. 

Akizungumzia jitihada ambazo Tanzania imezichukua katika kuzuia na kupambana na rushwa, Rais Samia amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA katika utoaji huduma za kijamii jambo lililosaidia kuepuka kukutana ana kwa ana baina ya watoaji na wapokeaji huduma huku akitoa mfano wa kutumia TEHAMA katika michakato ya zabuni, usajili wa biashara, namba ya mlipa kodi pamoja na maombi ya kuunganishiwa umeme. 

Katika hatua nyingine Rais Samia ameipongeza TAKUKURU, ZAECA, Asasi za Kiraia pamoja na Wadau mbalimbali kwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa hapa nchini.   

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Tanzania imepata heshima ya pekee ya kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Kupambana na Rushwa Barani Afrika huku akiahidi kuwa, yeye na Waziri wa Zanzibar mwenye dhamana ya utawala bora kuendelea kuzisimamia TAKUKURU na ZAECA ili ziweze kutekeleza wajibu wake kikamilifu. 

Ameongeza kuwa kupitia Maadhimisho hayo, Tanzania imeweza kupata uzoefu katika mapambano dhidi ya rushwa  nchini ambapo imepata fursa ya kujadili kwa pamoja mada mbalimbali akitolea mfano  wa mada ya utaifishwaji wa  mali za watuhumiwa waliopata mali hizo kupitia rushwa pamoja na mbinu mbalimbali za kupambana na rushwa kwa njia za kidigitali.  

"Tunakushukuru sana Mhe. Rais kwa dhamira na utashi wako katika mapambano dhidi ya rushwa ambayo umekuwa ukiyaongoza hapa nchini" amesema Mhe. Simbachawene. 

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika, Pascoal Antonio Joaquim amesema maadhimisho hayo yameweza kuainisha changamoto mbalimbali ambazo nchi za Afrika zimekuwa zikikabiliana nazo kwa kuhakikisha zinatafutiwa suluhu ya kudumu. 

Amesema ikiwa ni miaka 20 sasa tangu nchi za Afrika kuingia Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kupambana na Rushwa  zimeweza kulichukulia suala la rushwa kama ni kosa la jinai kwa kuanzisha taasisi mbalimbali na mifumo ya kisheria ya kuwapeleka Mahakamani wale wote wanaojihusisha nayo.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali wa taasisi za umma, sekta binafsi, wanafunzi na wananchi wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika ambayo yamefanyika leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC, jijini Arusha.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuzungumza na viongozi mbalimbali wa taasisi za umma, sekta binafsi, wanafunzi na wananchi wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika ambayo yamefanyika leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC, jijini Arusha.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) CP Salum Hamduni alipokuwa akielezea majukumu ya taasisi yake wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika ambayo yamefanyika leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC, jijini Arusha.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Afisa kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Bi. Johari Msirikale alipokuwa akielezea namna taasisi hiyo inavyopamba na rushwa wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika ambayo yamefanyika leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC, jijini Arusha.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akinyanyua tuzo aliyokabidhiwa na Bodi ya Ushauri ya Kupambana na Rushwa Afrika wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika ambayo yamefanyika leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC, jijini Arusha.


Sehemu ya Maafisa kutoka katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungmza nao wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika ambayo yamefanyika leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC, jijini Arusha.


Sehemu ya Maafisa kutoka katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungmza nao wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika ambayo yamefanyika leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC, jijini Arusha.


Sehemu ya Wanafunzi wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungmza nao wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika ambayo yamefanyika leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC, jijini Arusha.

 


 

No comments:

Post a Comment