Na. Veronica Mwafisi-Bagamoyo
Tarehe 15 Julai, 2023
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewapongeza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kwa kusimamia na kuwahudumia vizuri walengwa wa Mradi wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao kwa asilimia kubwa umeinua maisha ya wananchi wa eneo hilo.
Mhe. Kikwete ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF wa Kata ya Dunda, Kijiji cha Dunda katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
“Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora niwapongeze ninyi viongozi wa Halmashauri ya Bagamoyo kwa kujitoa kwenu katika kuwasimamia na kuwahudumia wananchi wa eneo hili la Bagamoyo,” Mhe. Kikwete amesema.
Mhe. Kikwete amesema kuwa, endapo halmashauri zote nchini Tanzania zitasimamia na kuratibu mradi wa TASAF kwa usahihi kama ambavyo halmashauri ya Bagamoyo inafanya, ifikapo mwaka 2026 nchi ya Tanzania itakuwa imeondokana na tatizo la wananchi kuwa na hali duni za maisha.
Aidha, Mhe. Kikwete amewataka wananchi na walengwa wa
halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kumuombea Rais Mhe. Dkt. Samia Hassan kwa
kuwa anafanya kazi kubwa ya kuhakikisha kila mwananchi anainuka kutoka katika
hali duni na kuwa na maisha bora.
Kwa upande wake, mlengwa wa TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Mwanahawa Sobbo ameishukuru TASAF kwa kumuinua kimaisha na kumuunganisha na vikundi ambavyo vimemsaidia kupata mkopo wa Halmashauri ya Wilaya ambao umewawezesha kununua machine ya boti inayofanya biashara na kuwaingizia kipato kikubwa.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani
Kikwete amehitimisha ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Pwani iliyolenga
kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili
watumishi hao pamoja na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete
akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF wa Kata ya Dunda, Kijiji cha Dunda
katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu
Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Sehemu
ya wananchi na walengwa wa TASAF wa Kata ya Dunda, Kijiji
cha Dunda, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani
Kikwete (hayupo pichani) wakati akizungumza nao alipokuwa kwenye ziara ya
kikazi iliyolenga
kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika halmashauri hiyo.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Shauri Selenda akitoa neno la
utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Ridhiwani Kikwete kuzungumza na wanachi na walengwa wa TASAF wakati wa ziara yake
ya kikazi katika Halmashauri hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya
TASAF.
Mlengwa wa TASAF, Bi. Mwanaheri Maulidi akitoa ushuhuda kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete namna TASAF ilivyomsaidia kuinua maisha yake wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitazama baadhi ya
bidhaa za walengwa wa TASAF katika Kata ya Dunda, Kijiji cha Dunda, Wilaya ya Bagamoyo
wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji
wa miradi ya TASAF.
No comments:
Post a Comment