Wednesday, July 12, 2023

VIONGOZI WA SERIKALI ZA VIJIJI WAHIMIZWA KUWEKA UWAZI KATIKA KUWATAMBUA WANAOSTAHILI KUINGIZWA KWENYE MPANGO WA KUNUSURU KAYA MASKINI ILI KUEPUSHA MALALAMIKO

Na. Veronica Mwafisi-Kisarawe

Tarehe 12 Julai, 2023

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema ni jukumu la Watendaji wa Serikali za Vijiji kuwatambua wananchi ambao wanastahili kuingizwa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia mikutano ya vijiji ili kuwepo na uwazi pamoja na kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi ambao wana vigezo vya kuingizwa.                 

Mhe. Kikwete ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF wa Kata ya Masaki, Kijiji cha Kisanga Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Mhe. Kikwete amesema kuwa, kuna baadhi ya wananchi ambao wanastahili kuingizwa kwenye mradi wa TASAF wenye sifa na vigezo lakini  kutokana na kutoitishwa mikutano ya kijiji hupelekea baadhi yao kukosa nafasi ya kuingizwa kwenye mradi huo, hivyo amewataka viongozi hao kuendesha mikutano ya mara kwa mara ili kuondoa malalamiko ambayo yanaweza kutokea.

Aidha, Mhe. Kikwete amesisitiza wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani amekuwa akijitahidi kuboresha maisha ya wananchi wake kwa maendeleo ya Taifa la Tanzania.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete anaendelea na ziara ya kikazi katika Mkoa wa Pwani kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao pamoja na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF.



Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Bw. Zuberi Kizwezwe akitoa utambulisho wa viongozi wa Kata ya Masaki, Kijiji cha Kisanga kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete kabla ya Naibu Waziri huyo kuzungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitazama shamba la kilimo cha mikorosho na miembe ambalo ni mradi wa walengwa wa TASAF katika Kijiji cha Kisanga wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akisalimiana na wananchi wa Kata ya Masaki, Kijiji cha Kisanga mara baada ya kuwasili katika eneo hilo kwa lengo la kuzungumza na wananchi na walengwa wa TASAF wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akimkabidhi fedha mlengwa wa TASAF, Bi. Zubeda Omari ili aweze kukamilisha ujenzi wa nyumba yake aliyoijenga kupitia ruzuku ya TASAF. 



No comments:

Post a Comment