Tuesday, July 4, 2023

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWATAKA MAKATIBU TAWALA WA WILAYA KUZINGATIA MIIKO NA MAADILI YA UTENDAJI

 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka Makatibu Tawala wa Wilaya zote Tanzania Bara kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, miiko na maadili ya utendaji kazi kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Julai 04, 2023 wakati akifungua semina elekezi kwa Makatibu Tawala wa Wilaya Jijini Dodoma.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema Makatibu Tawala hao hawana budi kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu yao huku akisisitiza kuwa misingi hiyo ndio chachu ya ujenzi wa taswira nzuri ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amewasisitiza Watendaji hao kuweka mikakati ambayo itabeba na kusimamia vizuri ajenda za kitaifa na kuhakikisha wanadhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma katika maeneo yao ya kazi na wanapobaini kuwepo kwa ubadhirifu wasisite kuchukua hatua.

Vilevile, amewataka kusimamia ipasavyo suala la nidhamu, maadili na uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma ili wawahudumie wananchi kikamilifu huku akiwasihi Watendaji hao kuwa mfano wa kuigwa katika jamii.

‘‘Nendeni huko mkatatue matatizo ya wananchi, toeni lugha ya staha na yenye matumaini mtakapokuwa mnawahudumia, kila mmoja wenu ajitahidi kuacha alama katika utendaji wake wa kazi’’ amesisitiza Waziri Mkuu

Akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua semina hiyo elekezi kwa Makatibu Tawala hao, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema lengo ya mafunzo hayo ni kuwaongezea weledi Watendaji hao ili kuimarisha utawala bora.

Amesisitiza kuwa mafunzo hayo watakayopewa ni ya kimkakati ambayo yataenda kuleta mapinduzi kwa Makatibu Tawala hao ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri katika ofisi zao kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita imekusudia.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Angela Kairuki amewataka Watendaji hao watimize majukumu yao ipasavyo na wahakikishe wanasimamia utekelezaji wa maagizo ya viongozi katika maeneo yao ya kazi.

Awali, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete alitoa wito kwa Watendaji hao kuhakikisha mafunzo wanayopatiwa wanakwenda kuyafanyia kazi katika maeneo yao.

Mafunzo hayo ya siku tatu yameandaliwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Taasisi ya UONGOZI huku yakiwakutanisha Makatibu Tawala wa Wilaya nchini.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa  akizungumza wakati akifungua Semina elekezi ya siku tatu kwa Makatibu Tawala wa Wilaya Tanzania Bara yaliyoanza leo Julai 4 hadi Julai 6, 2023  Jijini Dodoma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.


Sehemu ya Makatibu Tawala wa WilayaTanzania Bara wakimsikiliza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati akifungua Semina elekezi iliyoanza leo Julai 4 hadi Julai 6, 2023  Jijini Dodoma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.


Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwa ajili ya kufungua Semina elekezi iliyoanza leo Julai 4 hadi Julai 6, 2023 Jijini Dodoma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.


Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na Makatibu Tawala mara baada ya kufungua Semina elekezi ya  siku tatu  kwa Makatibu Tawala hao wa  WilayaTanzania Bara yaliyoanza leo Julai 4 hadi Julai 6, 2023  Jijini Dodoma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Ridhiwan Kikwete akizungumza na Makatibu Tawala kabla ya kumkaribisha Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, Mhe. Kassim majaliwa kufungua Semina elekezi kwa  Watendaji hao Jijini Dodoma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Juma Mkomi akizungumza na Makatibu Tawala kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete  wakati wa kufungua mafunzo  kwa Watendaji hao Jijini Dodoma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi kabla ya kufungua Semina elekezi ya siku tatu  kwa Makatibu Tawala wa Wilaya Tanzania Bara yaliyoanza leo Julai 4 hadi Julai 6, 2023  Jijini Dodoma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma wakimsikiliza Waziri Mkuu  Mhe. Kassim Majaliwa  wakati akifungua Semina elekezi ya Uongozi kwa Makatibu Tawala wa Wilaya Tanzania Bara  yaliyoanza leo Julai 4 hadi Julai 6, 2023  Jijini Dodoma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mkurugenzi wa idara ya Uendelezaji Taasisi, Bw. Nolasco Kipanda kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma  akitoa mada wakati akitoa Semina elekezi kwa Makatibu Tawala wa Wilaya Tanzania Bara  yaliyoanza leo Julai 4 hadi Julai 6, 2023  Jijini Dodoma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.


Mkurugenzi wa idara ya Utawala na Utumishi wa Umma, Bi. Felister Shuli kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma wa  akitoa mada wakati akitoa Semina elekezi kwa Makatibu Tawala wa Wilaya Tanzania Bara  yaliyoanza leo Julai 4 hadi Julai 6, 2023  Jijini Dodoma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.



No comments:

Post a Comment