Tuesday, February 28, 2023

MHE. JENISTA AWATAKA WATUMISHI WA OFISI YAKE KUTOA USHIRIKIANO WA KIUTENDAJI KWA VIONGOZI WAPYA ILI KUENDELEA KUUBORESHA UTUMISHI WA UMMA

 Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 28 Februari, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa watumishi wa ofisi yake kuendelea kutoa ushirikiano wa kiutendaji kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi walioteuliwa na kuapishwa jana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutumikia ofisi hiyo.

Mhe. Jenista ametoa wito huo leo jijini Dodoma, wakati wa hafla fupi ya kuwapokea viongozi hao walipowasili ofisini kwa ajili ya kuanza kazi rasmi mara baada ya kuapishwa jana na Rais wa Jamhuri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Jenista amesema ushirikiano kwa viongozi hao kutoka kwa watumishi utawawezesha kwa kiasi kikubwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kutoa mchango katika Utumishi wa Umma kama ilivyokusudiwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Jenista amesema, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imepata viongozi wenye sifa stahiki kwa ajili ya kuongeza nguvu ya kiutendaji, hivyo hatuna budi kuwapa ushirikiano wa kutosha ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu katika kufikia maono ya Rais wa Awamu ya Sita ya kuuboresha Utumishi wa Umma nchini.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, viongozi hao wateule wataendeleza pale walipoishia watangulizi wao katika kuujenga utumishi wa umma wenye uadilifu na unaowajibika kwa wananchi katika kutoa huduma bora.

Kwa upande wake, Naibu Waziri mteule, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa watumishi wote na kuongeza kuwa, atahakikisha anasimamia haki katika kufanya kazi.

Mhe. Ridhiwani amesema, moja ya jukumu lake ni kumsaidia Waziri wake Mhe. Jenista Mhagama kutekeleza jukumu la kusimamia utumishi wa umma na utawala bora kwani kwa kufanya hivyo atakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuujenga utumishi wa umma unaowajibika kwa wananchi kwa hiari.

Naye Katibu Mkuu mteule, Bw. Juma Mkomi ameahidi kutoa ushirikiano kwa watumishi wa ofisi yake na kuwaomba nao kumpatia ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu aliyopatiwa na Mhe. Rais ya kutoa mchango katika ustawi wa Utumishi wa Umma nchini.

Bw. Mkomi amemshukuru mtangulizi wake, Dkt. Laurean Ndumbaro kwa msingi alioujenga katika utumishi wa umma na kuahidi kuendelea kutumia busara zake katika kuuimarisha utumishi wa umma.

Akitoa neno la shukurani, Katibu Mkuu aliyemaliza muda wake, Dkt. Laurean Ndumbaro, amemshukuru Waziri Jenista Mhagama, Watendaji na watumishi wote wa Ofisi ya Rais-Utumishi kwa ushirikiano waliompatia wakati wa uongozi wake uliowezesha kutekeleza jukumu la kuusimamia utumishi wa umma.

Amewasihi watumishi hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa Viongozi wateule, kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili utumishi wa umma uwe na tija kwa ustawi wa taifa.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (wa pili kutoka kushoto) akipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake kutoka kwa mtangulizi wake, Dkt. Laurean Ndumbaro (wa kwanza kulia) mara baada ya Bw. Mkomi kuripoti rasmi katika ofisi hiyo iliyopo Mtumba jijini Dodoma. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (katikati) akizungumza na watumishi wa ofisi yake kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wake Mhe. Ridhiwani Kikwete (wa kwanza kulia) kuzungumza na watumishi hao mara baada ya kuripoti rasmi katika ofisi hizo zilizopo Mtumba jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bw. Juma Mkomi.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (wa pili kutoka kulia) akizungumza na watumishi wa ofisi hiyo mara baada ya kuripoti rasmi katika ofisi hizo zilizopo Mtumba jijini Dodoma baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan Kulia kwake ni Waziri wa Ofisi hiyo Mhe. Jenista Mhagama.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akizungumza na Menejimenti ya ofisi yake mara baada ya kuripoti rasmi katika ofisi hizo zilizopo Mtumba jijini Dodoma baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma aliyemaliza muda wake, Dkt. Laurean Ndumbaro (wa kwanza kulia) akitoa neno la shukurani kwa watumishi wa ofisi hiyo alipokuwa akiwaaga. Wengine ni viongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akimkaribisha Naibu Waziri wa ofisi yake, Mhe. Ridhiwani Kikwete mara baada ya kuripoti rasmi katika ofisi hizo zilizopo Mtumba jijini Dodoma baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akimkaribisha Katibu Mkuu wa ofisi yake Bw. Juma Mkomi mara baada ya kuripoti rasmi katika ofisi hizo zilizopo Mtumba jijini Dodoma baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI. Nyuma ya Mhe. Waziri Jenista ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akisalimiana na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maadili, Bi. Leila Mavika mara baada ya Naibu waziri huyo kuripoti rasmi katika ofisi hizo zilizopo Mtumba jijini Dodoma. 


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akisalimiana na watumishi wa ofisi hiyo mara baada ya kuripoti rasmi katika ofisi hizo zilizopo Mtumba jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama.


Sehemu ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati akiwakaribisha Naibu Waziri wa ofisi hiyo na Katibu Mkuu mara baada ya kuripoti rasmi katika ofisi hizo zilizopo Mtumba jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (meza kuu) akizungumza jambo na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (kushoto) mara baada ya Katibu Mkuu huyo kuripoti katika ofisi hizo Mtumba jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi.





 

Saturday, February 25, 2023

VIONGOZI MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA WATAKIWA KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOKWAMISHA WANANCHI KUPATA HUDUMA BORA

 Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 26 Februari, 2023

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika halmashauri kutatua changamoto zinazokwamisha wananchi kupata huduma bora pindi wanapofuata huduma katika maeneo yao ya kazi.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo jijini Dodoma, wakati akifunga kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichofanyika kwa siku tatu katika ukumbi wa Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali Mtumba.

Mhe. Ndejembi amesema, viongozi hao wanapaswa kukerwa na changamoto zinazowakabili wananchi pindi wanapofuata huduma katika maeneo yao ya kazi na kuchukua hatua stahiki ya kuwahimiza watendaji wanaowasimamia kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Ndejembi amewahimiza viongozi hao, ambao wengi wao wanatoka maeneo ya pembezoni kuhakikisha wanasimamia vema rasilimaliwatu ili wananchi wapate huduma bora, kwani wananchi wengi waishio pembezoni mwa nchi wanalazimika kutumia gharama kubwa kufuata huduma kwenye ofisi za makao makuu ya mikoa na halmashauri za wilaya.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka viongozi hao kutatua changamoto zinazowakabili watumishi ili wasiwe na sababu ya kutotoa huduma bora kwa wananchi na kuongeza kuwa, anaamini viongozi hao wanatambua wajibu wao katika kutatua kero za watumishi na wananchi kwa ujumla.

“Kuna changamoto ambazo mnahitaji kuwasikiliza tu watumishi au wananchi na kutoa majibu sahihi, lakini mmekuwa na tabia ya kukwepa jukumu hilo na kulielekeza kwa Katibu Mkuu-UTUMISHI jambo ambalo si sahihi kwani lipo ndani ya mamlaka zenu na uwezo wenu kiutendaji,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu wa Halmashauri ya Mji Handeni, Bw. Steven Bavu amesema watahakikisha wanatekeleza agizo la Mhe. Ndejembi la kutatua kero za wananchi katika maeneo yao ya kazi.

Naye, Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Bi. Judith Mahende amesema Mhe. Ndejembi amewahimiza kutatua kero za wananchi kwasababu katika Serikali za Mitaa ndio kuna wananchi wengi wanaowasilisha changamoto ili zitatuliwe, hivyo watatenga muda wa kuwatembelea na kuwasikiliza ili kutatua changamoto zinazowakabili.

Kikao kazi hicho kilicholenga kuhimiza uwajibikaji kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kilifunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Anjela Kairuki na kufungwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wakati akifunga kikao kazi cha viongozi hao jijini Dodoma kilicholenga kuboresha utendaji kazi wao.


Sehemu ya Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati akifunga kikao kazi chao jijini Dodoma kilicholenga kuboresha utendaji kazi wao.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kufunga kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kuboresha utendaji kazi katika Utumishi wa Umma.


Mkurugenzi Msaidizi wa Idara Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Sekretarieti ya Mkoa wa Singida, Bw. Pancras Kakwere ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa akitoa neno la shukrani mara baada ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kufunga kikao kazi kikao kazi chao kilicholenga kuboresha utendaji kazi wao.


Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu, Halmashauri ya Mji Handeni, Bw. Steven Bavu akielezea namna watakavyotekeleza maelekezo ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi aliyoyatoa wakati akifunga kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu katika Serikali za Mitaa kilicholenga kuboresha utendaji kazi wao.

 


Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu, Wilaya ya Rombo, Bi. Judith Mahende akiahidi kutekeleza maelekezo ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi aliyoyatoa wakati akfunga kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na Wakuu wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu katika Serikali za Mitaa kilicholenga kuboresha utendaji kazi wao.

 



Friday, February 24, 2023

MHE. NDEJEMBI AWAHIMIZA VIONGOZI NA WATENDAJI MIKOANI KUIUNGA MKONO SERIKALI KWA KUBUNI MBINU MBALIMBALI ZITAKAZOWAWEZESHA WALENGWA WA TASAF KUJIINUA KIUCHUMI

 Na. Veronica Mwafisi-Makambako

Tarehe 24 Februari, 2023

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi amewahimiza Viongozi na Watendaji mikoani kuiunga mkono Serikali kwa kubuni mbinu mbalimbali zitakazowawezesha walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kujiinua kiuchumi.

Mhe. Ndejembi amesema hayo wakati wa ziara yake yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Mji Makambako mkoani Njombe.

Mhe. Ndejembi amewahimiza viongozi na watendaji hao kufuatia Uongozi wa Mkoa wa Njombe ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka kubuni mbinu ya utekelezaji wa kilimo cha upandaji parachichi kwa kuwapatia miche ya parachichi walengwa hao ili kujiendeleza kimaisha.

Mhe. Ndejembi amesema kuwa, lengo la mradi wa TASAF ni kumuinua mwananchi kutoka kwenye hali duni ya maisha na kumfikisha katika hatua nyingine ya juu, hivyo ni vizuri mwananchi huyo akasaidiwa kwa kufanya shughuli za maendeleo ili aweze kujitegemea kiuchumi.

“Nina hakika kwa kupanda miche hii ya parachichi, kaya hizi za walengwa wa TASAF zitainuka kwa kujiongezea kipato na kumuwezesha mlengwa kuishi maisha bora,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi ametoa wito kwa walengwa hao wa TASAF wa Halmashauri ya Mji Makambako kutoa ushirikiano katika kutekeleza kilimo cha parachichi kwani kinalenga kuwanufaisha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka amesema, Mkoa wa Njombe unafaidika na kilimo cha parachichi kwani ndani ya miaka mitatu mkulima anaweza kuvuna, hivyo waliona wawasaidie walengwa wa TASAF kuwaandalia mazingira mazuri ya kujishughulisha na kilimo cha parachichi kwa lengo la kuwaongezea kipato.

Mhe. Mtaka amesema hayo yote yanatekelezwa kwa walengwa wa TASAF kwa lengo la kupunguza tatizo la umaskini nchini.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Njombe iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao pamoja na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF wa Halmashauri ya Mji Makambako wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri hiyo mkoani Njombe.


Baadhi ya wananchi na walengwa wa TASAF wa Halmashauri ya Mji Makambako wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri hiyo mkoani Njombe.


Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Halmashauri ya Mji Makambako wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Mji Makambako mkoani Njombe. 


Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. Augustino Ngude akitoa salamu za TASAF kwa wananchi na walengwa wa TASAF wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi katika Halmashauri ya Mji Makambako mkoani Njombe.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akisisitiza jambo mara baada ya kukabidhi miche kwa walengwa wa TASAF wa Halmashauri ya Mji Makambako wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri hiyo mkoani Njombe.


Mwonekano wa miche ya parachichi waliyopatiwa walengwa wa TASAF katika Halmashauri ya Mji Makambako mkoani Njombe.

 



Thursday, February 23, 2023

MHE. NDEJEMBI AWAASA WATUMISHI WA UMMA KUWAHUDUMIA VIZURI WANANCHI ILI KUJENGA TASWIRA NZURI YA SERIKALI KWA UMMA

 Na. Veronica E. Mwafisi-Njombe

Tarehe 23 Februari, 2023

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewaasa watumishi wa umma nchini kuwahudumia vizuri wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zitolewazo na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Mhe. Ndejembi wito huo kwa watumishi wa umma, wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Mji Njombe mkoani Njombe kilicholenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao katika halmashauri hiyo.

Mhe. Ndejembi amesema, kila mtumishi wa umma nchini akitimiza wajibu wake kuna uwezekano mkubwa wa kutatua matatizo ya wananchi kwani kila mtumishi wa umma kwa nafasi yake ni mwakilishi wa Serikali hivyo anapaswa kuilinda taswira ya Serikali kwa kutoa huduma nzuri kwa wananchi ili wananchi wajivunie uwepo wa serikali yao.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, watumishi wa umma wanapaswa kutoa huduma bora kwa wananchi kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesimamia na anaendelea kusimamia vema masilahi ya watumishi wote wa umma nchini, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kufanya kazi kwa bidii ikiwa ni sehemu ya kuthamini na kuunga mkono jitihada hizo za Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe, Mhe. Erasto Mpete amemshukuru Naibu Waziri Ndejembi kwa kufanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Mji Njombe ili kuhimiza uwajibikaji, kusikiliza na kutatua kero za watumishi wa halmashauri hiyo kitendo ambacho kimejenga ari na morali ya utendaji kazi wa watumishi wa umma katika halmashauri yake.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi anaendelea na ziara yake ya kikazi  katika Halmashauri ya Mji Njombe kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Halmashauri hiyo ya mji mkoani Njombe.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Mji Njombe, wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF katika Halmshauri hiyo ya mji mkoani Njombe.


Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Mji Njombe wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF katika Halmshauri hiyo mkoani Njombe.


Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Kissa Gwakisa akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuhimiza uwajibikaji, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF katika wilaya yake wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo katika Halmshauri ya Mji Njombe mkoani Njombe.


Mkuu wa Idara ya Utawala na Utumishi, Halmashauri ya Mji Njombe, Bi. Ester Zullu akisoma taarifa ya utumishi ya halmashauri hiyo ya mji kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF katika Halmshauri hiyo ya mji.


Mtumishi wa Halmashauri ya Mji Njombe, Dkt. Stephano Mbapila akiwasilisha hoja ya kiutumishi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF katika Halmshauri hiyo ya mji mkoani Njombe.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akisikiliza hoja iliyokuwa ikiwasilishwa na mtumishi wa Halmashauri ya Mji Njombe wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF katika Halmshauri hiyo ya mji mkoani Njombe.



MHE. JENISTA ATOA WITO KWA WANANCHI KUSHIRIKIANA NA TAKUKURU KUZUIA VITENDO VYA RUSHWA KWENYE MIRADI YA MAENDELEO

Na. James K. Mwanamyoto-Magu

Tarehe 23 Februari, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa wananchi katika maeneo yote ambayo miradi ya maendeleo ya TASAF inatekelezwa, kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika kuzuia vitendo vya rushwa ambavyo ndio visababishi vya miradi hiyo kutokamilika kwa wakati na hatimaye kuchelewesha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Jenista ametoa wito huo akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa Zahanati ya Kijiji cha Ihayabuyaga, Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza inayojengwa na TASAF kupitia ufadhili wa Umoja wa Nchi zinazosambaza Mafuta Duniani (OPEC).

Mhe. Jenista amewasisitiza wananchi kuwa mstari wa mbele katika usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo ikikamilika kwa wakati inawanufaisha kwa kuwapatia huduma bora kama ilivyokusudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Jenista amesema, Serikali imekusudia kila fedha ya mradi inayotolewa, itumike vizuri na ndio maana kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeanzisha programu maalum ya TAKUKURU RAFIKI aliyoizindua Disemba 20, 2022 jijini Dodoma ikilenga kuwashirikisha wananchi na wadau katika kuzuia vitendo vya rushwa nchini.

 “Kupitia TAKUKURU RAFIKI, wananchi wanakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa, hivyo tutoe taarifa ya viashiria au uwepo wa vitendo vya rushwa bila woga kwani TAKUKURU RAFIKI ipo kwa ajili hiyo,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, hivi sasa TAKUKURU RAFIKI ipo karibu na kila Mtanzania kwa lengo la kuhakikisha kila mradi unatekelezwa vizuri, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuitumia fursa ya TAKUKURU RAFIKI kulinda fedha za umma zinazotokana na kodi ambazo zinachangiwa na wananchi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Magu mkoani Mwanza, Mhe. Boniventura Kiswaga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga nyumba ya watumishi katika Zahanati ya Kijiji cha Ihayabuyaga kupitia fedha za TASAF ili kutatua changamoto ya wananchi kuchelewa kupatiwa huduma kutokana na watumishi wa zahanati hiyo kuishi mbali na kituo cha kazi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Mwanza iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya TASAF.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akitoa maelekezo ya ukamilishwaji wa miundombinu katika nyumba ya watumishi wa Zahanati ya Kijiji cha Ihayabuyaga, Halmashauri ya Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya TASAF wilayani humo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Kijiji cha Ihayabuyaga, Halmashauri ya Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya TASAF wilayani humo.


Sehemu ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Kijiji cha Ihayabuyaga, Halmashauri ya Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya TASAF wilayani humo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu mara baada ya kuwasili wilayani humo kwa ziara ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya TASAF wilayani humo.


Mbunge wa Jimbo la Magu mkoani Mwanza, Mhe. Boniventura Kiswaga akitoa salamu za shukrani kwa Serikali kujenga nyumba ya watumishi katika Zahanati ya Kijiji cha Ihayabuyaga kupitia fedha za TASAF ili kutatua changamoto ya wananchi kuchelewa kupatiwa huduma kutokana na watumishi wa zahanati hiyo kuishi mbali na kituo cha kazi.


Mwonekano wa nyumba ya watumishi wa Kituo cha Afya, inayojengwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Kijiji cha Ihayabuyaga, Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.


 

Wednesday, February 22, 2023

TASAF YAELEKEZWA KUJENGA WODI YA AKINA MAMA NA AKINA BABA KATIKA ZAHANATI YA LUSHAMBA ILI KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA

Na. James K. Mwanamyoto-Sengerema

Tarehe 22 Februari, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameulekeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kujenga wodi ya akina mama na akina baba kufuatia maombi ya wananchi wa kijiji hicho ambao wamekuwa wakipata adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo katika Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Zahanati ya Lushamba inayoboreshwa na TASAF mkoani Mwanza.

Mhe. Jenista amesema, kwa heshima ya wananchi wa Kijiji cha Lushamba, Serikali ya Awamu ya Sita kupitia TASAF itajenga wodi hizo mbili ya akina mama na akina baba mara baada ya kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Lushamba na miundombinu yake.

“Baada ya awamu ya pili ya ujenzi wa miradi ya Umoja wa Nchi zinazosambaza Mafuta Duniani (OPEC) kukamilika, TASAF hakikisheni mnajenga wodi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wanawake na wanaume watakaohitajika kulazwa katika zahanati hiyo ya Lushamba,” Mhe. Jenista amesisitiza

Ameongeza kuwa, fedha hizo za miradi ya OPEC zimepatikana kutokana na jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akihangaikia maendeleo ya nchi yake, hivyo ni vema kumuunga mkono katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

Akizungumzia adha wanayoipata wananchi wa Kijiji cha Lushamba katika kupata matibabu, Mhe. Jenista ameelekeza kukamilika haraka kwa Kituo cha Afya cha Lushamba ifikapo tarehe 31 Machi, 2023.

Ameongeza kuwa zahanati hiyo ikikamilika itawawezesha akina mama kupata huduma salama ya afya ya uzazi kwani watoto watakaozaliwa ni rasilimali muhimu itakayotoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Akizungumzia adha ya huduma ya afya wanayoipata, mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Lushamba, Bi. Monica Pawenzu amesema wamekuwa wakihangaika sana kupata huduma ya afya ya uzazi kwa kuingia gharama ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Bi. Pawenzu amemshukuru Mhe. Jenista kwa kuelekeza ukamilishaji wa zahanati pamoja na ujenzi wa wodi mbili ya akina mama na akina baba kwani itawawezesha kupata huduma za afya za uhakika na kwa gharama nafuu.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na mlengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji Lushamba, Kata ya Bulyaheke, Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo mkoani Mwanza.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisikiliza hoja ya mmoja wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha Lushamba, Kata ya Bulyaheke, Halmashauri ya Buchosa, wilayani Sengerema alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo mkoani Mwanza


Mwonekano wa Kituo cha Afya, kinachoendelea kujengwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Kijiji cha Lushamba, Kata ya Bulyaheke, Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwahimiza viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema kukamilisha mradi wa ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Chema wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Mwanza.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwasisitiza wanafunzi wa Shule ya Msingi Chema, Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema kusoma kwa bidii ili kuunga mkono jitihada za serikali za kujenga madarasa katika shule hiyo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akihimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wilayani Sengerema wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.

 

NYARAKA ZINAZOHIFADHIWA KATIKA KITUO CHA KUMBUKUMBU KANDA YA ZIWA ZINARAHISISHA UTENDAJI KAZI WA SHUGHULI ZA SERIKALI KATIKA KANDA HIYO-Mhe. Jenista

Na. James K. Mwanamyoto-Mwanza

Tarehe 22 Februari, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema kumbukumbu na nyaraka zinazohifadhiwa katika Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa zinarahisisha utendaji kazi wa shughuli za serikali za kila siku kwenye maeneo ya Kanda hiyo.

Mhe. Jenista amesema hayo jijini Mwanza wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa kituo hicho pamoja na viongozi na watendaji wa serikali kilicholenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa kituo hicho.

Mhe. Jenista amesema nyaraka ni uti wa mgongo wa utekelezaji wa majukumu ya serikali kwa kuwa maamuzi yote yanayofanywa na serikali yanategemea kumbukumbu na nyaraka zilizohifadhiwa kwa ajili ya rejea ya kiofisi.

Akifafanua zaidi kuhusiana na nyaraka zilizohifadhiwa katika kituo hicho cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa, Mhe, Jenista amesema, ameshuhudia baadhi ya kumbukumbu na nyaraka zilizohifadhiwa ambazo zinaeleza historia ya taifa letu kabla ya uhuru, wakati wa uhuru na baada ya uhuru na kuongeza kuwa nyaraka hizo ni urithi wa taifa letu.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, nyaraka hizo pia ni muhimu katika kutatua migogoro mbalimbali ikiwemo ya ardhi ambayo ipo na inaendelea kujitokeza katika jamii kwani zinaonyesha uthibitisho wa mipaka na uhalali wa umiliki wa ardhi.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa, Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi amesema kumbukumbu zinazohifadhiwa katika kituo hicho hupatikana kwa urahisi zinapohitajika kwa ajili ya rejea mbalimbali. 

Bw. Msiangi ametoa mfano wa majalada ya mashauri ya Mahakama ya Tanzania yaliyofungwa na kuhifadhiwa katika kituo hicho kuhitajika mara kwa mara kwa ajili ya rejea ya maamuzi ya mashauri mbalimbali na rufaa zinazowasilishwa kwenye mamlaka husika. 

Katika kuongeza ufanisi wa kiutendaji, Bw. Msiangi amesema kituo hicho kitaunganishwa na mfumo wa serikali mtandao ili kuwezesha nyaraka zitakazohifadhiwa kituoni kuwa katika mfumo wa kidijitali kwa lengo la kulinda nakala halisi na kurahisisha upatikanaji wake pindi zinapohitajika.

Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa kimekuwa msaada mkubwa kwa rejea ya kiofisi na uendeshaji wa shughuli mbalimbali za serikali katika Kanda ya Ziwa. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akionyeshwa moja ya nyaraka zilizoko katika Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa kilichoko jijini Mwanza wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa kituo hicho. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa na baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali jijini Mwanza (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma.  


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza jambo kwa watumishi wa Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa na baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali jijini Mwanza wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma.  


Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi, akitoa maelezo ya awali kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) kuhusu Kituo cha Kumbukumbu Kanda ya Ziwa kilichopo jijini Mwanza wakati wa ziara ya kikazo ya Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa kituo hicho.