Na. Veronica Mwafisi - Moshi
Tarehe 14 Oktoba, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa
watumishi wa umma nchini kutumia mfumo wa kielektroniki wa ushughulikiaji wa
malalamiko ya watumishi wa umma na wananchi katika utumishi wa umma (eMrejesho)
kuwasilisha malalamiko yao ambayo yamechukua muda mrefu kufanyiwa kazi na
waajiri wao ili yaweze kufanyiwa kazi kwa wakati na kuwawezesha watumishi hao
kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Mhe. Jenista ametoa wito huo kwa
watumishi wa umma wote nchini wakati akizungumza na watumishi wa Sekretarieti
ya Mkoa wa Kilimanjaro, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya
Wilaya ya Moshi akiwa kwenye ziara ya kikazi ya mkoani Kilimanjaro.
Mhe. Jenista amesema, mfumo wa
eMrejesho ni mfumo pekee unaochangia ushughulikiaji wa malalamiko kwa wakati na
kuuboresha utumishi wa umma kuwa uliotukuka, hivyo watumishi wa umma wanapoona
malalamiko yao yanachelewa kufanyiwa kazi katika vituo vyao vya kazi,
wayawasilishe Ofisi ya Rais-UTUMISHI kupitia mfumo huo.
Katika kuhakikisha watumishi
wanawasilisha malalamiko yao kupitia mfumo huo, Waziri Jenista amewasisitiza
Watendaji Serikalini kutoa taarifa kwa watumishi wa umma wote juu ya uwepo wa
mfumo huo ili wautumie katika kutatua changamoto zinazowakabili.
“Katibu Tawala nikuombe sana kuhakikisha
watumishi katika halmashauri zote wanapewa taarifa za mfumo wa eMrejesho ili
waufahamu na kuweza kuutumia kwa kuwasilisha malalamiko yao, maoni na hata
ushauri ili kuujenga utumishi wa umma,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe.
Jenista ameongeza kuwa mfumo huu umetengenezwa sio kwa ajili ya matumizi ya watumishi
wa umma pekee bali hata kwa wananchi ambao wanaweza kuutumia kwa kuwasilisha
changamoto zilizo katika maeneo wanayoishi akitolea mfano migogoro ya ardhi na
uhaba wa maji kwani kwa kufanya hivyo kutawapunguzia Viongozi Wakuu wa Kitaifa
kadhia ya kushughulikia malalamiko wanapokuwa katika ziara zao za kikazi kwani
yatakuwa yameshughulikiwa na maafisa husika katika taasisi.
Pamoja na uwepo wa mfumo wa eMrejesho, Mhe. Jenista amesema akiwa ndiye Waziri anayemsaidia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kusimamia utumishi wa umma na utawala bora anao mfumo unaojulikana kwa jila la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI ambao umeunganishwa na dawati la huduma kwa mteja ukilenga kutatua changamoto za kiutumishi na utawala bora.
Mhe. Jenista amefanya kikao kazi na
watumishi wa mkoa wa Kilimanjaro ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kukutana na
watumishi wa umma nchini kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua
changamoto zinazowakabili watumishi hao ili waweze kutoa huduma bora kwa
wananchi kwa ustawi wa taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama
akizungumza na Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Kilimanjaro, Halmashauri ya
Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi wakati wa ziara yake ya
kikazi mkoani Kilimanjaro iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi hao.
Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa
Kilimanjaro, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi
wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao
wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo mkoani Kilimanjaro iliyolenga kuhimiza
uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.
Afisa Tarafa Kata ya Moshi Magharibi,
Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Bw. Senzia Lushino akiwasilisha hoja kwa Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama wakati kikao kazi cha Waziri huyo na Watumishi wa Sekretarieti
ya Mkoa wa Kilimanjaro, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya
Wilaya ya Moshi kilicholenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi wa mkoa huo.
No comments:
Post a Comment