Na. Veronica Mwafisi - Arumeru
Tarehe 13 Oktoba, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ametoa
wito kwa wananchi wa Vijiji vya Karangai na Maweni, Halmashauri ya Wilaya ya
Meru kutumia hatimiliki za kimila walizonazo kufanya shughuli za maendeleo ili
kujikwamua kiuchumi.
Mhe. Jenista ametoa wito huo
mara baada ya kukagua na kuzindua masijali za ardhi za Vijiji vya Karangai na
Maweni katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru mkoani Arusha zilizojengwa na
Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA).
Mhe. Jenista amesema MKURABITA
imekuwa ikifanya kazi nzuri ya kurasimisha ardhi, lengo likiwa ni kuwasaidia
wananchi kufanya shughuli za maendeleo na kujikwamua kiuchumi.
“Kitendo cha MKURABITA kupima
na kukabidhi hatimiliki za kimila, tayari imeshakuondolea umaskini, hivyo ni
namna sasa ya wewe uliyenufaika na hatimiliki hiyo kufuata maelekezo ya
kuitumia kwa maendeleo yako kwani hati hiyo ni dhamana yako ya kupata mkopo,”
Mhe. Jenista amesisitiza
Mhe Jenista amewasisitiza
wananchi hao kutoogopa kukopa fedha kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo
kwani mtu akitaka kuwa na maendeleo hawezi kuepuka kukopa.
“Msigope kukopa kwani mikopo ndiyo
inayowasaidia wengi kuinuka kiuchumi na ndio maana Serikali imewarasimishia
ardhi ili mpate hati ambazo zitawasaidia kukopa na kufanya shughuli za
maendeleo ili lengo la serikali la kuona uchumi wa mtu mmoja mmoja unakua
linafikiwa.” Mhe. Jenista ameongeza.
Katika kuwawezesha wananchi
hao kukopa, Mhe. Jenista ameziomba taasisi za kifedha kuitikia wito wa serikali
wa kushusha riba hadi kufikia digitali moja.
Aidha, Mhe. Jenista amewataka
watumishi wa masijali za ardhi alizozizindua kutenda haki katika kuwahudumia
wananchi.
“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan
kupitia MKURABITA amewajengea ofisi nzuri hivyo mtumie ofisi hizo kuwahudumia
wananchi kwa kutenda haki, utendaji wenu wa kazi uwe tofauti na wengine,” Mhe.
Jenista amesisitiza na kuongeza kuwa shughuli zote zifanyike kwa uwazi ili
kutoipa rushwa nafasi.
Kwa upande wake, Mratibu wa
MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe amewasisitiza wananchi wa vijiji hivyo kutumia
masijala zilizozinduliwa kufanya shughuli za maendeleo.
“Lengo la kujengwa kwa
masijala hizi ni kufanya shughuli za maendeleo na sio vinginevyo, hivyo
mzitumie vizuri ili kuhakikisha maendeleo ya mmoja mmoja na taifa kwa ujumla
yanapatikana,” Dkt. Mgembe amesisitiza.
Mhe.
Jenista yuko mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na kuzindua masijala
katika Vijiji vya Karangai na Meru katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru, alizindua
pia Kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara na katika
Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisoma maandishi ya uzinduzi wa jengo la masijala ya ardhi lililojengwa na MKURABITA katika
Kijiji cha Maweni, Halmashauri
ya Wilaya ya Meru mkoani Arusha mara baada ya kuzindua rasmi masijala hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa
shughuli za MKURABITA katika Halmashauri hiyo. Wanaoshuhudia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha,
Mhe. John Mongella pamoja na watendaji wengine wa Serikali.
Mwonekano wa jengo la masijala ya ardhi lililojengwa na
MKURABITA katika Kijiji cha Karangai, Kata ya Kikwe, Halmashauri ya Wilaya ya
Meru mkoani Arusha lililozinduliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa
shughuli za MKURABITA katika Halmashauri hiyo.
Mwonekano wa jengo la masijala ya ardhi lililojengwa na
MKURABITA katika Kijiji cha Maweni, Kata ya Kikwe, Halmashauri ya Wilaya ya
Meru mkoani Arusha lililozinduliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa
shughuli za MKURABITA katika Halmashauri hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza
na wananchi wa Kijiji cha Karangai na Maweni, Kata ya Kikwe, Halmashauri ya Wilaya
ya Meru, mkoani Arusha wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua
utekelezaji wa shughuli za MKURABITA katika Halmashauri hiyo.
Wananchi wa Kijiji cha Karangai na Maweni, Halmashauri ya
Wilaya ya Meru mkoani Arusha wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo
pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara
yake ya kikazi ya Waziri Jenista iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za
MKURABITA katika Halmashauri hiyo.
Mkuu
wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella akitoa salamu za mkoa wake kabla ya
kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Karangai na Maweni,
Halmashauri ya Wilaya ya Meru wakati
wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista katika Halmashauri ya Meru iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za MKURABITA katika Halmashauri
hiyo.
Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa majukumu MKURABITA kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista iliyolenga kukagua
utekelezaji wa shughuli za MKURABITA katika Halmashauri Wilaya ya Meru.
No comments:
Post a Comment