Na. James K. Mwanamyoto - Lindi
Tarehe 11 Oktoba, 2022
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka
watumishi wa umma nchini kutoogopa kuwasilisha changamoto zinazowakabili kwa
kuwahofia waajiri kuwajengea chuki na kuwaahidi kuwa, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itawalinda kwasababu Mhe. Rais
Samia Suluhu Hassan anataka kupata mrejesho utakaoiwezesha Serikali kuujenga Utumishi
wa Umma wenye uadilifu na unaowajibika kwa masilahi ya taifa.
Mhe. Ndejembi ametoa wito huo
kwa watumishi wa umma nchini, wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na
watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi, Manispaa ya Lindi, Halmashauri ya
Wilaya ya Mtama na wa taasisi za umma mkoani Lindi.
“Sisi viongozi tunaomsaidia
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kusimamia Utumishi wa Umma tunapowatembelea msiogope
kuelezea changamoto zinazowakabili kwani tunakuja kuzitatua, hivyo tutawalinda
na iwapo mtaogopa mtajinyima fursa ya kuwasilisha changamoto zenu ili
zitatuliwe kama Mhe. Rais alivyoelekeza,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Mhe. Ndejembi amesema Ofisi ya
Rais-UTUMISHI haitosita kumchukulia hatua stahiki Afisa Utumishi au mwajiri
atakayebainika kumuonea mtumishi aliyejitokea kuwasilisha changamoto
zinazomkabili.
Akiwasilisha hoja kuhusu
watumishi wa umma kupata changamoto ya kubadilishiwa miundo ya kiutumishi (recategorization), mmoja wa watumishi wa
Idara ya Elimu Sekondari mkoani Lindi, Bw. Sharif Daudi Kiao amehoji ni kwanini
mtumishi aliyejiendeleza kielimu kwa ajili ya kuutumikia umma pindi anapomuomba
mwajiri kumbadilishia kada analazimika kushushwa mshahara wake ili apate sifa ya
kukitumikia cheo kipya.
Akitoa ufafanuzi kuhusiana na
hoja iliyowasilishwa na mtumishi huyo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ametoa ushauri
kwa watumishi wa umma nchini pindi wanapotaka kujiendeleza kielimu kuhakikisha
wanazingatia uhitaji wa mwajiri kwa wakati huo ili wakihitimu wawe na tija kiutendaji
ambayo inamshawishi mwajiri kumbadilishia
kada (recategorization) ili aweze
kutoa mchango katika Utumishi wa Umma.
Akizungumzia hoja ya mtumishi
anayeomba kubadilishiwa kada kulazimika kushushwa mshahara wake, Mhe. Ndejembi
ameeleza kuwa kwa watumishi wanaojiendeleza ndani ya kada zao kama vile Afisa
Kilimo Msaidizi (Diploma) kuwa Afisa Kilimo (Degree) wakibadilishwa kada
wanaombewa kibali cha mshahara binafsi, lakini kwa yule atakayeomba
kubadilishiwa kada kwa ajili ya kukidhi matilaba binafsi (job satisfication) atalazimika kuanza na cheo cha kuingilia na mshahara wa cheo kipya kwa kada husika na atakuwa
amekosa sifa ya kuombewa kibali cha mshahara binafsi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi yuko
mkoani Lindi kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku tatu, inayolenga kutatua
changamoto zinazowakabili watumishi wa umma mkoani humo ikiwa ni pamoja na kukagua
utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF) nchini.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb)
akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi, Manispaa ya Lindi na
wa taasisi za umma mkoani Lindi (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi
mkoani Lindi yenye lengo la kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.
Baadhi ya watumishi wa
Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi, Manispaa ya Lindi na wa taasisi za umma mkoani
Lindi wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara
yake ya kikazi mkoani Lindi iliyolenga kutatua changamoto zinazowakabili
watumishi wa umma.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe.
Shaibu Ndemanga akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi (Mb) kuzungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi,
Manispaa ya Lindi na wa taasisi za umma wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu
Waziri huyo mkoani Lindi yenye lengo la kutatua changamoto zinazowakabili watumishi
wa umma.
Mmoja wa watumishi wa Idara ya
Elimu Sekondari mkoani Lindi, Bw. Sharif Daudi Kiao akiwasilisha changamoto ya
kiutumishi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu
Waziri huyo mkoani Lindi iliyolenga kutatua changamoto zinazowakabili watumishi
wa umma mkoani humo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb)
akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa
wa Lindi, Manispaa ya Lindi na wa taasisi za umma mkoani humo wakati wa kikao
kazi chake na watumishi hao kilicholenga
kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (kulia)
akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Shaibu Ndemanga wakati wa kikao
kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi, Manispaa
ya Lindi na wa taasisi za umma kilicholenga kutatua changamoto zinazowakabili
watumishi wa umma mkoani Lindi.
No comments:
Post a Comment