Saturday, October 22, 2022

MAFUNZO YA VIONGOZI KUJITAMBUA KUIWEZESHA KAMATI YA USEMI KUSIMAMIA UTUMISHI WA UMMA UWE NA TIJA KWA MAENDELEO YA TAIFA

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 22 Oktoba, 2022

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema, mafunzo kuhusu uongozi unaojitambua yanayotolewa na Taasisi ya UONGOZI kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) yatawajengea uwezo wa kuisimamia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili watumishi wa umma nchini wawe na tija katika utendaji kazi na kutoa mchango kwa maendeleo ya taifa.

Mhe. Ndejembi amesema hayo leo jijini Dodoma, wakati akifungua mafunzo ya Sanaa ya Uongozi (The Art of Leadership) yanayotolewa kwa wajumbe wa Kamati ya USEMI kwa lengo la kuwajengea uwezo utakaosaidia kuwawezesha kusimamia vema utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

Mhe. Ndejembi amesema, mafunzo hayo yanayotolewa ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwataka viongozi kujitambua na kuwa na uwezo wa kufanya uchambuzi yakinifu katika masuala mbalimbali ambayo utekelezaji wake utakuwa na manufaa katika maendeleo ya taifa.

“Mafunzo haya yanayotolewa mahususi kwa kamati hii nyeti ya USEMI iliyopewa jukumu la kusimamia ofisi kuu mbili zilizopo chini ya Mhe. Rais Mwenyewe, ambazo ni Ofisi ya Rais-UTUMISHI na TAMISEMI zilizopewa dhamana ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati”, Mhe. Ndejembi amefafanua.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Michael Mwakamo amesema wamepewa mafunzo yanayowawezesha kutambua maana halisi ya uongozi, namna ya kutekeleza majukumu yao, namna ya kuwa wasikivu kwa wananchi wanaowaongoza ikiwa ni pamoja na kutambua umuhimu wa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

“Hakika haya ni mafunzo yenye tija kwa mustakabali wa uongozi wa taifa, na ikiwezekana mafunzo haya yaendelee kutolewa kwa viongozi wengine wa kisiasa na wanaotekeleza majukumu mengine ya kiserikali,” Mhe. Mwakamo amesisitiza.

Naye, Mjumbe wa Kamati ya USEMI ambaye pia ni Mbunge wa Urambo anayeshiriki mafunzo hayo ya uongozi, Mhe. Margaret Sitta amesema kuwa mafunzo waliyopatiwa yamewakumbusha wajibu wao kama wabunge na wajumbe wa kamati, hivyo watatumia elimu waliyoipata kutathmini utendaji kazi wao ili uwe na tija katika kuisaidia Serikali kutimiza lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi.

Akielekea lengo kuu la mafunzo hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uelewa wajumbe wa Kamati ya USEMI wa kutambua kuwa, uongozi ni sanaa hivyo kila kiongozi anapaswa kujipanga kikamilifu na kuwa na mfumo madhubuti utakaomuwezesha kutekeleza vema jukumu la uongozi.

Bw. Singo ameongeza kuwa, taasisi yake inatoa mafunzo yanayoainisha kuwa, kiongozi anapaswa kuwa na uwezo mkubwa wa kutafuta rasilimali (mobilization of resources), kuondoa vikwazo vinavyokwamisha maendeleo na kuwahamasisha watu anaowaongoza kuwa sehemu ya kuleta maendeleo.

Taasisi ya UONGOZI imekuwa mstari wa mbele katika kutoa mafunzo ya uongozi kwa makundi mbalimbali ya viongozi walio katika Utumishi wa Umma na sekta binafsi ili waweze kuwahudumia wananchi na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akieleza manufaa ya mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya UONGOZI kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa yanayofanyika jijini Dodoma.


Wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakifuatilia mafunzo ya uongozi yanayotolewa na Taasisi ya UONGOZI, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao.


Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Michael Mwakamo akitoa neno la utangulizi kabla ya kuanza kwa mafunzo ya uongozi yanayotolewa na Taasisi ya UONGOZI kwa wajumbe wa kamati hiyo jijini Dodoma.


Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo akielezea lengo kuu la mafunzo ya uongozi yanayotolewa na taasisi yake kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa yanayofanyika jijini Dodoma.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (kulia) akijadili jambo na mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Festo Sanga (kushoto) wakiwa kwenye mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya UONGOZI jijini Dodoma.


Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Margaret Sitta akieleza namna watakavyotumia ujuzi na elimu waliyoipata katika mafunzo ya uongozi yanayotolewa na Taasisi ya UONGOZI kwa Kamati hiyo jijini Dodoma. 


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakifuatilia mada kuhusu Uongozi Binafsi na Akili Hisia kwa njia ya Mtandao inayowasilishwa kwa njia ya mtandao na Bi. Zuhura Muro wa Taasisi ya UONGOZI.  


Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Bi. Mwantatu Khamis (katikati) akiwasilisha hoja kwa mwezeshaji wa mafunzo (hayupo pichani) wakati wa mafunzo ya uongozi yanayotolewa na Taasisi ya UONGOZI jijini Dodoma.



 

 

No comments:

Post a Comment