Wednesday, October 26, 2022

WAAJIRI WATAKIWA KUANDAA MADAWATI YA MSAADA ILI KUWEZESHA UTEKELEZAJI WA MAELEKEZO YA MHE. RAIS YA KUWAREJESHEA MICHANGO YAO WATUMISHI WA UMMA WALIOONDOLEWA KWA KUGHUSHI VYETI

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 26 Oktoba, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka waajiri katika taasisi za umma kuandaa madawati ya msaada yatakayowezesha kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuwarejeshea michango ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii watumishi walioondolewa kwenye utumishi wa umma kwa kosa la kughushi vyeti. 

Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dodoma, mara baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako kutangaza msamaha wa Rais wa kuwarejeshea michango watumishi walioondolewa kwa kosa la kughushi vyeti, Mhe. Mhagama amesema, Serikali inategemea madawati hayo yawe msaada kwa walengwa wa msamaha huo. 

Mhe. Mhagama amesema, madawati hayo yatakuwa msaada wa haraka kwa walengwa wa msamaha huo wa Mhe. Rais hasa katika kupata ufafanuzi, ujazaji wa nyaraka na kupokea nyaraka zinazohitajika kwa ajili ya kuwezesha mchakato wa urejeshwaji kwa michango hiyo kwa mujibu wa maelekezo. 

“Hatutegemei kusikia mlengwa wa msamaha huo atakapofika kwa mwajiri wake akutane na changamoto yoyote itakayokwamisha kurejeshewa michango aliyochangia katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kama ilivyoelekezwa na Mhe. Rais.” Mhe. Mhagama amesisitiza. 

Pamoja na maelekezo ya uanzishwaji wa madawati ya msaada, Mhe, Mhagama pia amewaelekeza waajiri kutoa ushirikiano kwa walengwa wa zoezi hilo, kuzingatia misingi ya utawala bora ili kuepusha uwezekano wa kutokea vitendo vya rushwa wakati wa kuratibu zoezi hilo. 

Katika kuhakikisha vitendo vya rushwa havijitokezi, Mhe. Mhagama ameilekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhakikisha inatumia mbinu za kimkakati ili walengwa wa msamaha huo wapate stahiki zao kwa mujibu wa maelekezo ya Mhe. Rais. 

Pia Mhe. Mhagama amewataka walengwa kuwa waaminifu kwa kuwasilisha nyaraka sahihi pindi zitakapohitajika kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa kurejeshwa michango yao. 

Aidha, katika kuhakikisha changamoto ya watumishi kuajiriwa kwa kutumia vyeti vya kughushi haijitokezi tena, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeuboresha Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara kubaini watakaowasilisha vyeti vya kughushi. 

“Mfumo huu unapeana taarifa na mifumo mbalimbali ukiwemo wa NIDA, TRA, RITA, NACTE na NECTA ili kupata taarifa sahihi za watumishi wa umma wote walioajiriwa nchini.” Mhe. Mhagama ameongeza. 

Amesema kitendo cha mifumo hiyo kupeana taarifa, kinawezesha mtumishi aliyeajiriwa serikalini kutambulika kwa njia tano ambazo ni jina la mtumishi, cheki namba, picha yake, alama za vidole na namba ya kitambulisho cha uraia. 

Mhe. Mhagama ametoa wito kwa waajiri wote nchini na taasisi zinazoshughulika na kuajiri kuwa makini wakati wa mchakato wa ajira na kuhakikisha tatizo la watumishi wenye vyeti vya kughushi halijitokezi. 

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia watumishi waliondolewa kwenye utumishi wa umma kwa kughushi vyeti warejeshewe michango waliyokatwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambapo PSSSF ni asilimia 5 na NSSF asilimia 10. 

Wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Mei Mosi 2022, Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (TUCTA) liliwasilisha ombi kwa Mhe. Rais la kuangalia namna ya kuwafuta jasho watumishi waliolitumikia taifa kabla ya kuondolewa kwa kosa la kughushi vyeti.   


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akitoa maelekezo kwa waajiri kupitia vyombo vya habari kuhusu kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuwarejeshea michango ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii watumishi walioondolewa kwenye utumishi wa umma kwa kosa la kughushi vyeti.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu msamaha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wa kuwarejeshea michango ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii watumishi walioondolewa kwenye utumishi wa umma kwa kosa la kughushi vyeti.


Sehemu ya waajiri na Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (hawapo pichani) wakati wa mkutano vya vyombo vya habari leo jijini Dodoma kuhusu maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuwarejeshea michango ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii watumishi walioondolewa kwenye utumishi wa umma kwa kosa la kughushi vyeti.

 

Sehemu ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (hawapo pichani) wakati wa mkutano vya vyombo vya habari leo jijini Dodoma kuhusu maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuwarejeshea michango ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii watumishi walioondolewa kwenye utumishi wa umma kwa kosa la kughushi vyeti.

 

 

 

No comments:

Post a Comment