Na. Veronica Mwafisi-Arusha
Tarehe 11 Oktoba, 2022.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa wafanyabiashara ndogondogo mkoani Arusha kukitumia Kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara kilichoanzishwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jijiji la Arusha ili kukuza biashara zao na kuongeza pato la taifa nchini.
Mhe. Jenista ameyasema hayo wakati akizindua rasmi kituo hicho
kilichopo katika Kata ya Kati, Mtaa wa Pangani, Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Mhe. Jenista amesema kituo hicho kimeanzishwa mahususi kwa ajili
ya kuwasaidia wajasiriamali hao kujifunza mambo mbalimbali pamoja na kupatiwa
mbinu tofauti za kibiashara hivyo ni fursa kwao kukitembelea ili kupata huduma
hiyo.
“Kituo hiki kitasaidia kurasimisha biashara zenu na kuweza
kutambulika na taasisi za kifedha ili muweze kupata mikopo katika taasisi hizo
kwa lengo la kuinua biashara zenu kwa maendeleo yenu binafsi na taifa kwa
ujumla,” Mhe. Jenista amesisitiza
Katika kuhakikisha wajasiriamali hao wanapata huduma bora katika
kituo hicho, Waziri Jenista amezitaka taasisi zote zinazotoa huduma jumuishi
kushiriki kikamilifu kutoa huduma ili wafanyabiashara hao wasipate kadhia
wanapoenda kupata huduma katika kituo hicho.
“Serikali kupitia MKURABITA imetumia fedha nyingi kuanzisha
kituo hicho kikubwa chenye ubora, hivyo taasisi zote jumuishi zinatakiwa zitoe
huduma na kuondoa kadhia kwa wafanyabiashara hao kwa kuwapatia huduma
inayostahili kama ilivyokusudiwa,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Ameongeza kuwa maono ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona wamiliki
wa ardhi na biashara ndogondogo wanapiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kupata
mikopo ya kuanzisha shughuli mbalimbali za kuwaongezea kipato.
Aidha, Mhe. Jenista amewataka watumishi wote wanaotoa huduma
katika kituo hicho kuzingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu yao ili
kutoa huduma bora kwa walengwa wanaopata huduma katika kituo hicho.
“Kila mtumishi wa umma atakayefanya kazi katika kituo hicho
atekeleze majukumu yake kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, tunataka
watumishi wote wawe mfano wa kituo hiki na wananchi waone umuhimu wa kazi
zinazofanywa na watumishi hao wa Jiji la Arusha,” Mhe. Jenista ameongeza.
Kwa upande wake, Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe
amemhakikishia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kushirikiana
na Halmashauri ya Jiji la Arusha katika mambo mbalimbali ya kuwawezesha
wafanyabiashara hao ikiwemo katika kutoa mafunzo ili waweze kuendeleza biashara
zao.
Kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara kimeanzishwa ili kuwasaidia na kuwarahisishia wafanyabiashara wa Jiji la Arusha kupata huduma zote za ushauri wa biashara pamoja na kupata mahitaji yote ya kibiashara katika sehemu moja.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifurahi
pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Said Mtanda (kushoto) na Watendaji
wengine wa Serikali mara baada ya Waziri Jenista kuzindua rasmi kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara kilichopo
katika Kata ya Kati, Mtaa wa Pangani Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza
na baadhi ya watumishi wanaotoa huduma katika kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara
kilichopo katika Kata ya Kati, Mtaa wa Pangani Halmashauri ya Jiji la Arusha
mara baada ya Waziri huyo kuzindua rasmi kituo hicho.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza
na wajasiriamali wanaopata huduma katika kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara
kilichopo katika Kata ya Kati, Mtaa wa Pangani Halmashauri ya Jiji la Arusha
alipokuwa
akizindua rasmi kituo hicho akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua
utekelezaji wa shughuli za MKURABITA mkoani Arusha.
Baadhi ya wajasiriamali
wanaopata huduma katika kituo Jumuishi
cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara kilichopo katika Kata ya Kati, Mtaa
wa Pangani Halmashauri ya Jiji la Arusha wakimsikiliza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akizungumza nao mara baada ya Waziri huyo
kuzindua rasmi kituo Jumuishi
cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara mkoani Arusha.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe.
Said Mtanda akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama
kuzindua rasmi kituo Jumuishi cha
Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara kilichopo katika Kata ya Kati, Mtaa wa
Pangani Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la
Arusha, Bw. Hargeney Chitukuro akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara
kilichopo katika Kata ya Kati, Mtaa wa Pangani Halmashauri ya Jiji la Arusha kabla
ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzindua rasmi kituo hicho.
Mratibu wa Mpango wa
Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Dkt.
Seraphia Mgembe akielezea majukumu ya taasisi yake kabla ya Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista
Mhagama kuzindua kituo Jumuishi
cha Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara kilichopo katika Kata ya Kati, Mtaa
wa Pangani Halmashauri ya Jiji la Arusha mkoani Arusha.
No comments:
Post a Comment