Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 24 Oktoba, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani amedhamiria kuendelea kutoa kipaumbele cha kuwapatia mafunzo viongozi ili kuwajengea uwezo kiutendaji, utakaowawezesha kumsaidia vema jukumu la kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo.
Mhe. Mhagama ameeleza dhamira hiyo
ya Mhe. Rais, wakati akifunga mafunzo ya Sanaa ya Uongozi (The Art of Leadership) kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge na
Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) yaliyotolewa na Taasisi ya UONGOZI jijini
Dodoma.
Mhe. Mhagama amesema, mara baada ya
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuapa na kuanza kulitumikia taifa, moja ya eneo
ambalo alielekeza lipewe kipaumbele ni kutoa mafunzo kwa viongozi akitambua
kuwa mafunzo ndio njia pekee ya kuwawezesha viongozi kuwa na ufanisi
kiutendaji, hivyo ofisi yake imetekeleza kwa vitendo agizo hilo kwa kuwapatia
mafunzo wajumbe wa kamati ya USEMI.
“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ana
maono na ndio maana anatambua kuwa sisi tuliopewa dhamana ya kuwa viongozi
tunahitaji kujengewa uwezo ili kupata ujuzi utakaoendana na mazingira yaliyopo
ikiwa ni pamoja na kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia,” Mhe. Mhagama
amefafanua.
Kwa upande wake, mmoja wa Wajumbe wa
Kamati ya USEMI, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Makete, Mhe. Festo Sanga amesema
toka awe Mbunge hajawahi kupata mafunzo mazuri ya uongozi kama ambayo Taasisi
ya UONGOZI imewapatia kwani yamemjengea uelewa kwenye eneo la akili hisia (emotional intelligence) utakaomuwezesha kuzungumza
vizuri na wananchi na kupokea yale ambayo wananchi anaowaongoza wanahitaji
kutekelezewa.
“Mafunzo haya kama Mbunge na Mjumbe wa
kamati ya USEMI yamekuwa na manufaa makubwa kwani yamenipatia elimu ya namna ya
kuisaidia Serikali katika ufuataliaji wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, pamoja na kusimamia matumizi ya fedha za umma ambazo Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikizitoa
katika maeneo mbalimbali nchini ili kuleta maendeleo,” Mhe. Sanga amesisitiza.
Naye, Dkt. Alice Kaijage (Mb) ambaye
pia ni Mjumbe wa Kamati ya USEMI amesema kuwa, kwa ujumla wajumbe wote wa
kamati ya USEMI waliopatiwa mafunzo wameridhika na maudhui ya mafunzo na
kushauri yaendelee kutolewa kwa muda mrefu zaidi ili viongozi wapate ujuzi
utakaowaongezea ufanisi kiutendaji.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) wamepatiwa Mafunzo ya Sanaa ya Uongozi (The Art of Leadership) na Taasisi ya UONGOZI kwa muda wa siku mbili, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuitaka taasisi hiyo kuendelea kuwajengea uwezo viongozi ili wawe na tija katika maendeleo ya taifa.
Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista
Mhagama akifunga mafunzo ya Sanaa ya Uongozi (The Art of Leadership) kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge na
Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) yaliyotolewa na Taasisi ya UONGOZI jijini
Dodoma.
Kaimu Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Michael
Mwakamo (wa kwanza kushoto) akiwa na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya USEMI,
wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati Waziri huyo akifunga
mafunzo ya Sanaa ya Uongozi (The Art of
Leadership) yaliyotolewa na Taasisi ya UONGOZI kwa wajumbe wa kamati hiyo
jijini Dodoma.
Sehemu ya Wajumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI)
wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (aliyesimama) wakati waziri huyo akifunga
mafunzo ya Sanaa ya Uongozi (The Art of
Leadership) yaliyotolewa na Taasisi ya UONGOZI jijini Dodoma.
Mjumbe wa Kamati ya USEMI ambaye ni
Mbunge wa Jimbo la Makete, Mhe. Festo Sanga akieleza faida ya mafunzo ya Sanaa
ya Uongozi (The Art of Leadership),
waliyopatiwa na Taasisi ya UONGOZI jijini Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo
wa kiutendaji.
Mjumbe wa Kamati ya USEMI, Dkt. Alice Kaijage akieleza namna wajumbe wa Kamati ya USEMI walivyonufaika na Mafunzo ya Sanaa ya Uongozi (The Art of Leadership), waliyopatiwa na Taasisi ya UONGOZI jijini Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji.
Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista
Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya USEMI na baadhi ya
Watendaji wa Serikali, mara baada ya waziri huyo kufunga mafunzo ya Sanaa ya
Uongozi (The Art of Leadership)
yaliyotolewa na Taasisi ya UONGOZI kwa wajumbe wa kamati hiyo jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment