Na. Veronica Mwafisi - Arumeru
Tarehe 13 Oktoba, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amezitaka Kamati za Nidhamu kuhitimisha kwa wakati mashauri ya kinidhamu ya watumishi wa umma ili kuipunguzia serikali gharama kubwa ambayo imekuwa ikiingia kwa kuwalipa mishahara watumishi waliopoteza sifa ya kuendelea kuwa watumishi, ikiwa ni pamoja kupunguza gharama za kuendesha mashauri ya kinidhamu kwa muda mrefu.
Akizungumza na watumishi wa Halmashauri
za Wilaya ya Arusha na Meru wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Arumeru,
Mhe. Jenista amesema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuwalipa watumishi
ambao pengine baada ya kuhitimishwa kwa mashauri yao wanatakiwa kuondolewa
katika utumishi wa umma.
“Naziagiza Kamati za Nidhamu zote
nchini kuhakikisha mashauri yote ya kinidhamu ya watumishi wa umma
yanahitimishwa kwa wakati kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo ili
haki itendeke, kwani Serikali imekuwa ikiwagharamia watumishi ambao wameshapoteza
sifa ya kuwa watumishi wa umma na wanalazimika kutofanya kazi yoyote pindi
wanaposubiri hatma ya mashauri yao,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Ameongeza kuwa, mtumishi anapotuhumiwa kuwa na kosa la kinidhamu
na kufunguliwa shauri la kinidhamu, hatima
yake ni aidha kuondolewa katika utumishi wa umma au kuendelea na utumishi wa
umma, hivyo ni vema Kamati ziwe na utamaduni wa kuharakisha mchakato wa
uendeshaji wa mashauri ya kinidhamu ili kuokoa fedha za serikali ambazo
zitakazotumika kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.
Aidha, Mhe. Jenista amewataka
watumishi wa umma kufanya kazi kwa uadilifu, ubunifu na weledi katika utekelezaji
wa majukumu yao ili kuwa na tija katika maendeleo ya taifa.
Waziri Jenista amesema, kila
mtumishi kwa nafasi yake anao uwezo mkubwa wa kuitumia taaluma yake katika
kuchangia maendeleo ya taifa na ndio maana Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea
kuboresha maslahi yao ili kuwajengea morali ya utendaji kazi.
“Lengo la Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuona taifa lake linapata
maendeleo makubwa na sisi watumishi kila mmoja kwa nafasi yake tunaowajibu wa
kuhakikisha tunatimiza ndoto ya Mhe. Rais,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Akimkaribisha Mhe. Jenista
kuzungumza na watumishi wa Halmashauri za Wilaya ya Arusha na Meru, Mkuu wa
Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella amemshukuru na kumpongeza Mhe. Jenista kwa
kuwa na utaratibu wa kufanya vikao kazi na watumishi wa umma ili kutatua changamoto
zao na kuhimiza uwajibikaji.
Mhe. Mongella amesema, mafanikio
makubwa yanayopatikana nchini hivisasa yanatokana na uchapakazi wa watumishi wa
umma ambao unachagizwa na watumishi kuridhishwa na namna serikali inavyowajali
hivyo kuwaongezea morali ya kufanya kazi kwa bidii.
Waziri Jenista ameendelea na ziara
yake ya kikazi mkoani Arusha inayolenga kutatua changamoto zinazowakabili,
kuhimiza uwajibikaji na kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa
Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza
na Watumishi wa Halmashauri za Wilaya ya Arusha na Meru wakati wa ziara yake ya
kikazi wilayani Arumeru iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi hao.
Watumishi wa Halmashauri za Wilaya
ya Arusha na Meru wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani)
alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo wilayani
Arumeru iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili
watumishi hao.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John
Mongella akitoa salamu za mkoa wake kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza
na watumishi wa Halmashauri za Wilaya ya Arusha na Meru wakati wa ziara ya
kikazi ya Mhe. Jenista wilayani Arumeru iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na
kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa wilayani humo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiteta
na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe.
Jenista wilayani Arumeru iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi wa wilaya hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
ya Wilaya ya Meru, Bi. Zainab Makwinya akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
halmashauri yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe.
Jenista wilayani Arumeru iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi wa wilaya hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
ya Wilaya ya Arusha, Bw. Seleman Msumi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
halmashauri yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe.
Jenista wilayani Arumeru iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi wa wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment