Wednesday, October 26, 2022

WATUMISHI WA TAKUKURU WILAYANI KILOLO WATAKIWA KUITUNZA OFISI MPYA NA MIUNDOMBINU YAKE ILI ITUMIKE KUPAMBANA NA RUSHWA

 Na. Veronica E. Mwafisi-Kilolo

Tarehe 26 Oktoba, 2022

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Kilolo kulitunza jengo jipya la ofisi pamoja na miundombinu yake ili litumike kikamilifu katika kuzuia na kupambana na rushwa kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita imekusudia.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo kwa watumishi wa TAKUKURU wilayani Kilolo, wakati akikagua ujenzi wa jengo jipya la TAKUKURU linalojengwa katika halmashauri hiyo kwa lengo la kuwawekea mazingira rafiki yatakayowawezesha kutekeleza ipasavyo jukumu la kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa.

“Ninawaasa mtakaokuwa mnatumia ofisi hii, muitunze ofisi na miundombinu yake na wala msiwasubiri viongozi wa ngazi za juu kutoka makao makuu ya TAKUKURU waje kuwaelekeza namna ya kuitunza kwani jukumu la kuitunza ni lenu,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni amekuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya watumishi wa TAKUKURU hivyo ni jukumu la watumishi hao wa TAKUKURU wilayani kilolo kuunga mkono jitihada za kiongozi wao kwa kuitunza ofisi hiyo mpya na miundombinu yake ili iwe na tija katika kuendeleza mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa kwenye wilaya hiyo.

Aidha, Mhe. Ndejembi ameushukuru uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kwa kuwapatia TAKUKURU eneo la kujenga ofisi ambayo kwa kiasi kikubwa, itasaidia kuongeza ufanisi wa watumishi wa TAKUKURU kiutendaji.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa jengo hilo litakaloimarisha utekelezaji wa jukumu la kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa wilayani Kilolo.

Ameongeza kuwa, ujenzi wa jengo hilo utasaidia kuweka mazingira rafiki kwa wananchi wa Kilolo kupata huduma za jamii kwa wakati, bila kuombwa au kutoa rushwa.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amefanya ukaguzi wa jengo jipya la TAKUKURU wilayani Kilolo ili kujiridhisha na maendeleo ya ujenzi huo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la TAKUKURU katika halmashauri hiyo.

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la TAKUKURU katika halmashauri hiyo.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akikagua miundombinu ya jengo jipya la TAKUKURU katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, akiwa kwenye ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo. Wengine ni Viongozi na watumishi wa TAKUKURU wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo.


Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye akitoa taarifa ya ujenzi wa Ofisi mpya ya TAKUKURU wilayani ya Kilolo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi hiyo wilayani humo. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akitoa maelekezo kwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye, wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Kilolo. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Bw. Peres Magiri.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na watumishi wa TAKUKURU mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo jipya la ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Bw. Peres Magiri na Kushoto kwake ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye.


Mwonekano wa jengo jipya la ofisi ya TAKUKURU wilayani Kilolo.

 



No comments:

Post a Comment