Na James K. Mwanamyoto-Nyasa
Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imeahidi
kuzinufaisha kaya zote maskini nchini baada ya kuridhishwa na namna wananchi katika
vijiji vilivyonufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini walivyoboresha
maisha yao na kujikwamua katika lindi la umaskini liliokuwa likiwakabili.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) wakati
akizungumza na wanufaika na wananchi wa kijiji cha Nangombo wilayani Nyasa
akiwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango huo wilayani
humo.
Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, iwapo wanufaika wasingetumia ruzuku
vizuri kuboresha maisha, Serikali isingesita kusimamisha utekelezaji wa Mpango huu wa Kunusuru Kaya Maskini nchini.
“Hongereni wanufaika wa TASAF kijiji cha Nangombo na maeneo mengine kwa
kutumia ruzuku kuboresha maisha yenu, kujenga nyumba bora, kununua vifaa vya
shule kwa ajili ya watoto na kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi," Mhe.
Mkuchika amepongeza.
Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imeridhika na
mafanikio yaliyopatikana, hivyo itaendeleza vita dhidi ya umaskini, lengo
likiwa ni kuboresha maisha ya kaya zote maskini nchini.
Akiwasilisha taarifa ya kijiji cha Nangombo kuhusu utekelezaji wa Mpango
wa Kunusuru Kaya Maskini, Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Bw. Joseph P. Ngogi
amesema watoto 66 wa shule wananufaika na ruzuku inayotolewa hivyo imeongeza mahudhurio
shuleni na kliniki kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, aidha kaya
65 zimeboresha makazi yao kwa kujenga ama kukarabati na kuezeka kwa bati.
Mmoja wa wanufaika wa Mpango wa TASAF kijiji cha Nangombo, Bi. Mariana
Mkwaila amesema ruzuku anayoipata imemuwezesha kuwanunulia watoto wake sare za
shule, viatu na madaftari ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba kubwa ambayo
anatarajia kuizeka kwa bati hivi karibuni.
Naye, Bi. Elizabeth Damian amesema, alikuwa akiishi maisha ya kimaskini
kwenye nyumba ya nyasi kabla ya kuingizwa kwenye Mpango, lakini baada ya kuanza
kupokea ruzuku ameweza kufuga kuku, mbuzi na kufyatua tofali zilizomuwezesha
kujenga nyumba iliyoezekwa kwa bati.
Mhe. Mkuchika amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa
kuitembelea Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji
kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
wilayani humo.
Mnufaika wa TASAF wa Kijiji
cha Nangombo wilayani Nyasa, Bi. Elizabeth Damiani akitoa shuhuda ya namna
alivyonufaika na ruzuku anayoipata kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
katika kijiji hicho.
|
No comments:
Post a Comment