Saturday, October 5, 2019

WATENDAJI SERIKALINI WATAKIWA KUTENDA HAKI WAKATI WA UJAZAJI WA FOMU ZA OPRAS ZA WATUMISHI ILI KUEPUKA KUSHUSHA ARI YA UTENDAJI KAZI

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Simiyu  (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Msingi Bariadi Alliance mkoani Simiyu


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Msingi Bariadi Alliance mkoani Simiyu


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mataka (kushoto) akimkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) alipotembelea ofisini kwake kabla ya kikao kazi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Simiyu kilichofanyika katika  Shule ya Msingi Bariadi Alliance mkoani Simiyu.




Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (kushoto) akiteta jambo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini wakati wa kikao kazi kati yake na Watumishi wa Mkoa wa Simiyu  kilichofanyika katika  Shule ya Msingi Bariadi Alliance mkoani Simiyu.




Katibu Msaidizi Ajira na Nidhamu, Tume ya Utumishi wa Umma Bi. Celina Maongezi akiwasilisha mada, wakati wa kikao kazi kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb), Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma na Watumishi wa Mkoa wa Simiyu  kilichofanyika katika  Shule ya Msingi Bariadi Alliance mkoani Simiyu.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini akitoa ufafanuzi wa hoja, wakati wa kikao kazi kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (kushoto), Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma na Watumishi wa Mkoa wa Simiyu  kilichofanyika katika  Shule ya Msingi Bariadi Alliance mkoani Simiyu.



Na Happiness Shayo- SIMIYU (Bariadi)

Serikali imewataka Watendaji katika taasisi za umma kuacha vitendo vya upendeleo wakati wa ujazaji wa fomu za OPRAS kwa watumishi wa umma nchini ili kupima utendaji kazi wao, lengo likiwa ni kuepuka kushusha morali ya utendaji kazi kwa watumishi hao.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa umma mkoani Simiyu kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Msingi Bariadi Alliance mkoani humo.

 “Hakikisheni mnajaza fomu za OPRAS kiuhalisia bila upendeleo ili kila mtumishi apate haki yake anayostahili, epukeni kuwakatisha tamaa  watumishi wanaofanya kazi kwa bidii” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.

Dkt. Mwanjelwa ameweka bayana kuwa, watumishi wanaofanya kazi pamoja wanajuana kiutendaji, hivyo si jambo zuri kwa mtendaji kumpendelea mtumishi wakati wa ujazaji wa fomu za OPRAS.

“Serikali inahitaji OPRAS ambayo itaziba kabisa mianya ya upendeleo”, Dkt. Mwanjelwa amehimiza.

Aidha, Dkt. Mwanjelwa amefafanua kuwa, ujazaji wa fomu za OPRAS unatakiwa uzingatie uchapakazi wa mtumishi ikiwa ni pamoja na tabia na mwenendo wa mtumishi kwa ujumla.

“Kuwa mtumishi wa umma ni pamoja na kuwa na mwenendo bora. Mtumishi mwenye mwenendo mbaya hafai kuwa katika utumishi wa umma”, Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.

Dkt. Mwanjelwa amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa kutoa mafunzo ya OPRAS kwa watumishi wa mkoani humo na kuwataka kuendelea kuwaelimisha watumishi ili kila mtumishi atambue haki na wajibu wake.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho, Mkaguzi Mkuu wa Nje wa mkoa huo, Bw. Costantine Mabirika amemshukuru Dkt. Mary Mwanjelwa kwa kutoa elimu na maagizo ya kiutendaji, hivyo ameahidi kuwa yatatekelezwa ipasavyo ili kuboresha utendaji kazi wao.

Kikao kazi hicho ni muendelezo wa ziara ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) mkoani Simiyu yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watendaji na watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.



No comments:

Post a Comment