Na
James K. Mwanamyoto, Songea
11
Oktoba, 2019
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt.
(Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) amewapongeza Watumishi wa Umma wa Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa kutoa msaada wa fedha, sabuni za kufulia na mafuta
ya kula kwa watoto yatima wa kituo cha Swako kilichopo Songea mjini kwani
wameonyesha taswira nzuri ya utumishi wa umma kwa wananchi ambao ndio walengwa
wakuu wa huduma zitolewazo na taasisi za Serikali.
Mhe. Mkuchika ametoa pongezi
hizo alipokutana na Watumishi wa Umma kwenye ziara yake ya kikazi yenye lengo
la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na kukagua
utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani humo.
Akikabidhi msaada huo kwa
niaba ya watumishi hao, Mhe. Mkuchika amewashukuru watumishi waliochanga fedha
hizo na kutoa mahitaji mengine ambayo yamekuwa ni faraja kwa watoto hao.
“Msaada mlioutoa utakuwa ni
chachu ya kujenga ustawi wa watoto hao ili hapo baadae waweze kuwa na mchango
katika maendeleo ya taifa, na ndio maana mmemuona mlezi wa kituo hicho
amefurahi sana baada ya kupokea msaada wenu”, Mhe. Mkuchika amesisitiza.
Msaada
walioutoa watumishi hao ni mwendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro ya
kuzitaka taasisi za umma nchini kuadhimisha
Wiki ya Utumishi wa umma mwaka huu kwa kushiriki masuala ya kijamii ili kujenga
uhusiano mzuri na wananchi.
Aidha, Mhe. Mkuchika
amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Christina Mndeme na Katibu Tawala wa
Mkoa huo, Prof. Riziki Shemdoe kwa kuratibu vema utekelezaji wa maelekezo ya
ofisi yake katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu kwani pamoja
na kutekeleza maagizo mengine wakati wa wiki hiyo ambayo huadhimishwa tarehe 16
hadi 23 Juni kila mwaka lakini waliona pia ni vema wakawasilisha msaada kwa
watoto yatima .
Awali, Katibu Tawala Mkoa wa
Ruvuma, Prof. Riziki Shemdoe alimueleza Mhe. Mkuchika namna watumishi wa
Sekrekarieti ya Mkoa wa Ruvuma walivyojitoa kuchanga fedha hizo na kuhakikisha
wanashiriki kikamilifu shughuli za ustawi wa kijamii ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma nchini.
Mhe. Mkuchika anaendelea na
ziara ya kikazi mkoani Ruvuma yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi
wa umma, ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini mkoani humo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George
H. Mkuchika (aliyesimama) akiwa katika kikao kazi na watumishi wa Sekretarieti
ya Mkoa wa Ruvuma na Halmashauri ya Wilaya ya Songea kilichofanyika mjini
Songea kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
|
No comments:
Post a Comment