Na: Mwandishi Wetu, Dodoma
Tarehe 27 Januari, 2026
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete amezindua bodi ya ushauri
ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) na kuitaka ihakikishe inaisimamia Mamlaka
hiyo vyema na kutoa ushirikiano kwa menejimenti katika utatuzi wa changamoto
zinazokwamisha utekelezaji wa majukumu yake.
Mhe. Kikwete ametoa
wito huo leo Januari 27,2026.alipokuwa akizindua Bodi ya Ushauri ya e-GA katika ukumbi wa
mikutano wa ofisi hiyo iliyopo
Mtumba - Jijini Dodoma.
Mhe. Kikwete amempongeza
Dkt. Mussa Kissaka kwa kuteuliwa na Rais kwa mara ya pili kuwa Mwenyekiti wa
Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Serikali Mtandao na kumhakikishia ushirikiano wa
dhati ili kutimiza malengo ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya ujenzi wa
Serikali Mtadao yenye tija.
“Ninafahamu Mamlaka
imekuwa ikipata changamoto katika utekelezaji wa majukumu yake hasa pale taasisi
zinaposhindwa kutekeleza sheria, kanuni, viwango na miongozo ya serikali
mtandao, hivyo wekeni mikakati bora ya kudhibiti jambo hilo” alisisitiza Mhe.
Kikwete.
Aidha, aliongeza kuwa
moja ya mambo ambayo watumishi wa umma bado wanakiuka kwa makusudi au kwa kutofahamu
ni suala la kutumia anuani za baruapepe ambazo sio za Serikali katika kutuma au
kupokea taarifa za kiofisi jambo ambalo linasababisha kuvuja kwa siri za
Serikali.
Pia, alisisitiza kuwa
kila Wizara, Idara zinazojitegemea, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatakiwa
kutumia anuani za baruapepe za Kiserikali zilizo kwenye utaratibu wa .go.tz, .gov, au .org katika kutuma au
kupokea taarifa za kiofisi kwa njia ya baruapepe vinginevyo Sheria ichukue
mkondo wake.
Vile vile, Mhe. Kikwete
ametumia fursa hiyo kumtakia kila la kheri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika siku hii ya kuzaliwa kwake. Aidha,
amemuombea dua kwa Mwenyezi Mungu ili amjalie Rais kheri, afya njema na umri
mrefu ili aone wananchi wanavyonufaika na yale aliyoyaanzisha na kuyatekeleza
kwa manufaa ya taifa.
Mhe. Kikwete amepanda mti wa muembe ikiwa ni ishara ya kumpongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika siku yake ya kuzaliwa. Mti huo umepandwa katika eneo
la Ofisi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mtumba- Dodoma, tarehe 27
Januari, 2026.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (Kushoto) akiwasili katika Ofisi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kazi ya kuzindua Bodi ya Ushauri na kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi hizo zilizopo Mtumba- Dodoma, tarehe 27 Januari, 2026. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa eGA Eng. Benedict Ndomba.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (Kulia) akielekea kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) inayojengwa Mtumba, Dodoma. Kushoto ni Mkurugenzi wa e-GA Eng. Benedict Ndomba.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete akipanda mti wa muembe ikiwa ni ishara ya kumpongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika siku yake ya kuzaliwa. Mti huo umepandwa katika eneo la Ofisi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mtumba- Dodoma, tarehe 27 Januari, 2026. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa eGA Eng. Benedict Ndomba.
No comments:
Post a Comment