Na Eric Amani Dodoma, Tanzania
Naibu Waziri Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Mhe. Regina Qwaray, ametoa wito kwa watumishi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma kuimarisha ushirikiano na mshikamano katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Qwaray ametoa wito huo leo Januari 05, 2026 alipokuwa akizungumza na watumishi wa idara hiyo wakati wa ziara ya kikazi katika Idara hiyo akisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu miongoni mwa watumishi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha huduma za umma zinatolewa kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
Amesema kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha utendaji kazi katika utumishi wa umma, hivyo ni wajibu wa watumishi kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi, uzalendo na kwa kushirikiana ili kufikia malengo ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Msingi wa utumishi wa umma ni ushirikiano, kujutuma kwa bidii na kuweka maslahi ya mwananchi mbele. Ushirikiano wetu utaongeza ufanisi na kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali yao,” amesema Mhe. Qwaray.
Aidha, amewahimiza watumishi kuendelea kuzingatia maadili, nidhamu na miongozo ya utumishi wa umma pamoja na kutumia vyema rasilimali zilizopo katika kuwahudumia wananchi kwa haki na usawa.
Kwa upande wao, watumishi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma wameahidi kuendelea kushirikiana na kutekeleza majukumu yao kwa bidii na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi matarajio ya wananchi.
![]() |
Mkurugenzi
Msaidizi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma Bi. Verediana Ngahega akijitambulisha
kwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
Regina Qwaray (hayupo pichani) katika kikao kazi Januari 5, 2026 Dodoma
Tanzania |





No comments:
Post a Comment