Na. Antonia Mbwambo - Manyara
Tarehe 8 Januari, 2026
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray amewataka watumishi wa Umma kuwa wazalendo na wenye kutanguliza maslahi ya taifa mbele na kufanya kazi kwa weledi, maarifa na ujuzi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Qwaray ameyasema hayo leo Januari 8, 2026 Mkoani Manyara wakati akizungumza na watumishi wa umma ngazi ya Mkoa, Halmashauri ya Mji wa Babati na Hamashauri ya Wilaya ya Babati wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi.
Aliongeza kuwa, Waajiri wote wa Taasisi za Umma wanatakiwa kuweka kipaumbele katika kushughulikia changamoto zinazowakabili watumishi waliopo chini yao ikiwa ni pamoja na madai ya kupandishwa vyeo na malimbikizo ya mishahara.
“Ukiona mtumishi wa umma anaenda Wizarani kwa ajili ya kufuatilia utatuzi wa changamoto zake za kiutumishi, ujue viongozi kwa ngazi ya Mkoa, Mji na Halmashauri hawawajibiki ipasavyo” alisema Mhe. Qwaray.
Hivyo, ametoa wito kwa viongozi wa ngazi hizo kuwajibika kwa kuwasaidia watumishi walio chini yao kupata haki na stahiki zao kwa wakati ili wao waendelee kutekeleza wajibu wao wa kuwahudumia wananchi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia Mhe. Qwaray amewataka watumishi kuzingatia Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma ambazo zinaelekeza tabia na mienendo ambayo mtumishi anapaswa kuwa nayo anapokuwa anatoa huduma katika eneo lake la kazi.
Aidha, amesisitiza matumizi ya mifumo iliyopo na inayotumika katika kushughulikia masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwemo maombi ya uhamisho na likizo ili kuendana na teknolojia iliyopo kwa lengo la kuwa na utendaji unaozingatia muda na usawa.
Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray (hayupo pichani) wakati wa kikao na watumishi hao leo tarehe 8 Januari, 2026 katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Ayalagaya.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara Bw. Robert Makala David Lusako,Mwalimu Mkuu katika shule ya Msingi Sawe iliyopo mjini Babati Mkoani Manyara, akiuliza swali kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray kuhusu changamoto wanazokumbana nazo kama watumishi wa umma wakati wa kikao na watumishi hao kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Halmashauri ya Mji wa Babati leo tarehe 8 Disemba, 2025
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray (alie katikati) akiwasili katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Manyara kwa ziara ya kikazi leo tarehe 8 Januari, 2026.
No comments:
Post a Comment