Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma
|
na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani
Kikwete akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi chake na Menejimenti ya
Watumishi Housing Investments (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi katika
taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam. |
![]() |
Kaimu Mkurugenzi wa Watumishi Housing
Investments (WHI) Bw. Sephania Solomon akiwasilisha taarifa
ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Ridhiwani Kikwete katika taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam. |
![]() |
| Sehemu ya Menejimenti ya Watumishi Housing Investments wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete alipokuwa akizungumza nao katika kikao kazi cha Waziri huyo na Menejimenti hiyo jijini Dar es Salaam. |
Na Eric Amani-Dar es Salaam
Tarehe 27 Novemba, 2025
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete
ameitaka Menejimenti ya Watumishi Housing Investments (WHI) kuwaeleza wananchi
mafanikio yaliyopatikana kwani Serikali imekuwa ikifanya mambo mengi na makubwa lakini wananchi hawajui.
“Mnafanya kazi nzuri sana ya ujenzi
wa makazi ya Watumishi wa Umma na Wananchi na uwekezaji kupitia Faida Fund,
lakini wananchi hawajui, wa kuwaambia wananchi ni sisi, tuwaambie, tuangalie
namna ya kutangaza ili wajue” Mhe. Kikwete amesisitiza.
Mhe. Kikwete ametoa maelekezo hayo
leo tarehe 27.11. 2025 akiwa kwenye mwendelezo wa ziara ya kikazi katika
taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora ambapo leo ametembelea Watumishi Housing Investments (WHI) jijini
Dar es Salaam.
Amesema suala la ujenzi wa makazi ya
Watumishi wa Umma ni muhimu ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia
wananchi kwa utulivu na kuweza kuwabakisha watumishi hao katika maeneo yao ya
kazi kwani kila mtu anatamani kuishi kwenye mazingira rafiki.
Amesema pamoja na ujenzi wa makazi ya
Watumishi, WHI inapaswa kutumia teknolojia ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu
na zenye ubora ili Watumishi waweze kununua na kuongeza kuwa kipaumbele kiwe kwenye
mikoa ya pembezoni.
“Simamieni msingi ya uanzishwaji wa
Taasisi hii wa kujenga nyumba za watumishi kwa gharama nafuu, tufikirie nje ya
boksi ili kupata fedha za kujenga nyumba za kutosha na kufikia malengo ya
Serikali ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi badala ya kutegemea zaidi
Serikali, bajeti ya
Serikali iwe kichocheo tu,” Mhe.
Kikwete amesisitiza. “Mmeyafanya mengi yenye ubunifu, tunaona, mnastahili
pongezi kwa mliyoyafanya, kwa mfano kuanzisha Mfuko wa Uwekezaji (Faida Fund)
ni ubunifu mzuri, tuendelee kusimamia msingi wa uanzishwaji wa mfuko huu, tujitahidi
kutoa elimu ili Watumishi wa Umma wengi zaidi na wananchi wawekeze katika Mfuko
huu kwa maisha yao ya sasa na ya baadae pindi wanapohitimisha utumishi wao,”
ameongeza.
Amesema ni matamanio ya Rais Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona Watumishi wa Umma wanaishi kwenye mazingira
mazuri kama ambavyo amekuwa akisisitiza anataka watumishi waishi vizuri ili
kuweza kuwahudumia wananchi kwa ubora, “tutafsiri maono yake kwa kuyafanyia kazi,”
ameongeza.
Ametoa mfano kuwa WHI inaweza kuingia
mkataba wa ujenzi kwa kutumia Halmashauri zenye makusanyo makubwa ya mapato na
kujenga nyumba za watumishi, “angalieni Halmashauri inaweza kuchangia kiasi
gani na ninyi kiasi gani maana Halmashauri hawawezi kujenga nyumba, muingie katika
makubaliano kuona namna gani mnaweza kutekeleza mpango wenu.” Amesisitiza.
Mhe. Kikwete amesema ni wakati sasa
wa kuambiana ukweli na sio kuoneeana aibu, “nimeletwa kuja kusaidiana nanyi ili
pale mnapokwama tusonge mbele, ndio jukumu lililonileta hapa, tunatamani kuona
mabadiliko yanaonekana, tuongeze kasi ya wawekezaji katika Mfuko huu wa Faida Fund
kwa kujitangaza zaidi,” amesisitiza.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu
Mkuu-UTUMISHI, Bw. Nolasco Kipanda, akitoa neno la utangulizi kabla ya
kumkaribisha Waziri kuzungumza na Menejimenti ya WHI amesema kitendo cha Waziri
kufanya ziara katika taasisi zilizo chini ya Ofisi yake ni fursa kubwa kwa Watendaji
wa taasisi hizo kuboresha utendaji.
“Mhe. Waziri amerudi kwa kofia
nyingine ya juu zaidi hivyo, kutembelea taasisi zilizo chini ya Ofisi yake ni
fundisho kwa Viongozi wa Taasisi na hata kwetu sote kwani tunapata fursa ya
kusikiliza matamanio yake ili kuona namna bora ya kufanya vizuri zaidi katika
utekelezaji wa majukumu yetu kwa ustawi wa taifa.” Bw. Kipanda ameongeza.
Amesema kila anachozungumza Mhe.
Waziri kinagusa Watumishi wa Umma na wananchi akitolea mfano wa ujenzi wa
makazi ya watumishi na uwekezaji kupitia Mfuko wa Faida Fund kuwa ni kazi yake
ya kisera.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji,
Kaimu Mkurugenzi wa Watumishi Housing Investments (WHI) Bw. Sephania Solomon
amemshukuru Mhe. Kikwete kwa ushauri na maelekezo aliyoyatoa ambapo ameahidi kuyafanyia
kazi.





No comments:
Post a Comment