Wednesday, November 26, 2025

SEKRETARIETI YA MAADILI MNAYO MAMLAKA YA KUFUATILIA UKIUKWAJI WA MAADILI YA VIONGOZI NCHINI, FANYENI HIVYO BILA KUONEA MTU”- Mhe. Ridhiwani Kikwete

Na Eric Amani-Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameitaka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuchunguza na kufuatilia kwa kina ukiukwaji wa maadili kwa Viongozi wa Umma ili kuwa na taifa lenye uadilifu kwa ustawi wa taifa.

“Ninyi ndio wenye mamlaka ya kusema ukweli, fanyeni kazi iliyoanzisha chombo hiki, semeni ukweli bila kuogopa mtu wala kuonea mtu, chukueni hatua inapobainika kuna ukiukwaji wa maadili kwa yale yanayowahusu, shirikianeni na Taasisi simamizi za Maadili, ambayo hayawahusu pelekeni kwenye taasisi husika.”ameongeza Mhe. Kikwete.

Akiwa katika ziara ya kikazi leo katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi jijini Dodoma, Mhe. Kikwete amesema Serikali imelenga kupunguza mmomonyoko wa maadili katika taifa, hivyo Sekretarieti ya Maadili inao wajibu mkubwa kuhakikisha jambo hili linatekelezeka kwa ufasaha.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete amewataka Viongozi wa Umma wote kuhakikisha wanakamilisha ujazaji wa Matamko kwa Njia ya Mtandao (ODS) kabla ya tarehe 31 Disemba na kuwasilisha kwa utaratibu uliopangwa.

Aidha, ameisisitiza Sekretarieti ya Maadili kuendelea kutoa elimu ya ujazaji wa ODS ili Viongozi waelewe kwa kina na kuwarahisishia katika ujazaji, na kuwataka wataalam wa TEHAMA kushughulikia changamoto za mfumo na kupokea maoni na mapendekezo ya kuboresha mfumo huo.

Ukweli ni kuwa Dunia yetu imebadilika, tunaenda na Teknolojia, Kutokufahamu matumizi ya kompyuta isiwe kigezo cha kutojaza Matamko kwa Njia ya Mtandao,” ameongeza Mhe. Kikwete.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray ameomba ushirikiano kwa taasisi hiyo ili waweze kutekeleza majukumu kwa umoja.

“Hongereni kwa kazi mnayoifanya, tumekuja kwa utambulisho, binafsi mimi ni mgeni kuliko Waziri wangu, kikubwa ninachohitaji kutoka kwenu ni ushirikiano katika kujifunza ili tuweze kufanya kazi yenye tija kwa taifa.” Mhe. Qwaray amesisitiza.

Akitoa neno la shukrani, Kamishna wa Maadili, Mhe. Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi amemshukuru Waziri Kikwete pamoja Naibu Waziri kwa kuona umuhimu wa kwatembelea na kutoa maelekezo ya kuboresha utendaji.

“Mhe. Waziri tunashukuru kwa kututembelea, mimi pamoja na wenzangu tumepokea ushauri na maelekezo uliyotupatia, tunaahidi kuyafanyia kazi na kwenye changamoto tutakushirikisha.” ameongeza

   Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwa katika kikao na Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kikazi katika taasisi hiyo leo jijini Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray.

   Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kikazi katika taasisi hiyo leo jijini Dodoma. 

    Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete kuzungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kikazi katika taasisi hiyo leo jijini Dodoma. 

   Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kikazi katika taasisi hiyo leo jijini Dodoma. 


   Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akifurahia jambo na Kamishna wa Maadili, Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi alipowasili katika taasisi hiyo leo jijini Dodoma kwa ajili ya ziara ya kikazi. 

    Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray akikaribishwa na Kamishna wa Maadili, Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa ajili ya kikao kazi na Watumishi wa taasisi hiyo leo jijini Dodoma. 

    Sehemu ya Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi katika taasisi hiyo leo jijini Dodoma.

   Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akiteta na Kamishna wa Maadili, Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi kwenye kikao kazi chake na Viongozi na Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kikazi katika taasisi hiyo leo jijini Dodoma. 



   Kamishna wa Maadili, Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete na Watumishi wa taasisi hiyo leo jijini Dodoma


  
  

   Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mara baada ya kikao kazi chake na Watumishi hao leo jijini Dodoma. Wa pili kulia walioketi ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray na Wa pili kushoto walioketi ni Kamishna wa Maadili, Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi.



No comments:

Post a Comment