Monday, November 17, 2025

MHE. KIKWETE ATOA WITO KWA WATUMISHI WA UMMA KUONGEZA KASI YA UWAJIBIKAJI ILI KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI

 Na. Antonia Mbwambo-Dodoma

Tarehe 18 Novemba, 2025

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka watumishi wa Ofisi hiyo kuwa tayari kufanya kazi kwa kasi na kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni aliahidi mambo mengi na anatamani matokeo yaonekane kwa wananchi ndani ya muda mfupi, hivyo tunatakiwa kuongeza kasi na kukamilisha ahadi zake kwa wakati” alisema Mhe. Kikwete.

Waziri Kikwete aliyasema hayo alipokuwa akiongea na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Menejimenti ya Ofisi hiyo Novemba 18, 2025  wakati wa makabidhiano ya Ofisi hiyo Mtumba Jijini Dodoma.

Mhe. Ridhiwani amesema Serikali inaendelea kuboresha Utumishi wa Umma ili kumkomboa mwananchi na changamoto ya upatikanaji wa huduma bora.

Pia, Mhe. Kikwete amesema anatambua uhitaji mkubwa wa Watanzania hasa kwenye suala la ajira na kuelezea mkakati mkubwa utakaofanywa na Serikali katika kutatua changamoto ya ajira kwa Watanzania.

Kwa upande wake Naibu Waziri Mhe. Regina Qwaray amewasisitiza watumishi wa Ofisi hiyo kutoa ushirikiano kwa viongozi na watumishi wengine katika utendaji huku kila mmoja akitambua nafasi na thamani ya mwingine ili kufikia malengo ya Serikali ya utoaji wa huduma bora kwa ustawi wa taifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Menejimenti na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo (hawapo pichani) tarehe 18 Novemba, 2025 baada ya kukabidhiwa Ofisi na aliyekuwa Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati wa makabidhiano yaliyofanyika Mtumba Jijini Dodoma.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray akisalimiana na sehemu ya Watumishi wa Ofisi hiyo mara baada ya kuripoti rasmi ofisini hapo tarehe 18 Novemba, 2025 Mtumba Jijini Dodoma mara baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (aliyesimama) akitoa neno la utangulizi wakati wa makabidhiano ya Viongozi wateule wa ofisi hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete na Naibu Waziri wa ofisi hiyo Mhe. Regina Qwaray yaliyofanyika tarehe 18 Novemba, 2025 Jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi (watatu kutoka kulia) akimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao mara baada ya kukabidhiwa ofisi Mtumba Jijini Dodoma. Wengine ni baadhi ya Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya ofisi hiyo ambao ni Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dr. Ernest Mabonesho (wa Kwanza kulia) na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Mick Kiliba.


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi (aliyevaa miwani) akimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza na Menejimenti na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo baada ya Waziri huyo kukabidhiwa Ofisi tarehe 18 Novemba, 2025 Jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (wa tatu kulia) akikabidhiwa Nyaraka za Ofisi na aliyekuwa Waziri wa Ofisi hiyo Mh. Boniface George Simbachawene (wa pili kulia) wakati wa makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika tarehe 18 Novemba, 2025 Jijini Dodoma.


Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakisubiri kumpokea Waziri wa ofisi hiyo Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) kabla ya kuwasili katika ofisi hiyo iliyopo Mtumba jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (wa pili kutoka kushoto mstari wa kwanza) akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Idara na Vitengo mara baada ya kuwasili katika ofisi hiyo iliyopo Mtumba jijini Dodoma. 


Sehemu ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakisubiri kumpokea Waziri wa ofisi hiyo Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) kabla ya kuwasili katika ofisi hiyo zilizopo Mtumba jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (wa pili kutoka kushoto mstari wa kwanza) akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi Wasaidizi baada ya kuwasili katika ofisi hiyo iliyopo Mtumba jijini Dodoma.






No comments:

Post a Comment