Tuesday, September 29, 2026

MICHEZO NI MOJA YA NGUZO KATIKA UJENZI WA OFISI YA UMMA – WAZIRI KIKWETE

Na Eric Amani, Kilimanjaro

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amesema michezo ni moja ya nguzo muhimu katika kujenga utumishi wa umma wenye afya, mshikamano na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Mhe. Kikwete ameyasema hayo leo Septemba 29, 2026 alipowatembelea wanamichezo wa Utumishi Sports Club (Utumishi SC) mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya kuwapa moyo, hamasa na motisha wakati wakiendelea na hatua ya 16 Bora ya Mashindano ya Shirikisho la Michezo na Sanaa za Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2026.

Katika ziara hiyo, Waziri Kikwete amewapongeza wanamichezo wa Utumishi SC kwa kufanya vizuri katika hatua za awali za mashindano hayo na kufanikiwa kufuzu hatua ya 16 Bora, akiwataka kuendelea kuwa na nidhamu, mshikamano na kujituma ili kuwakilisha Ofisi ya Rais – Utumishi kwa heshima.

Amesema michezo ina nafasi kubwa katika kuwaunganisha watumishi wa umma, kujenga mahusiano mazuri kazini, kuimarisha afya pamoja na kuongeza ari na morali ya utendaji kazi.

“Michezo ni moja ya nguzo katika ujenzi wa Ofisi ya Umma. Inasaidia kujenga afya, umoja, mshikamano na mahusiano mazuri baina ya watumishi, jambo ambalo lina mchango katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi,” amesema Mhe. Kikwete.

Aidha, Waziri Kikwete amewataka wanamichezo hao kutumia mashindano hayo kama fursa ya kuonesha nidhamu, uzalendo na uwezo wao, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimu wapinzani na kuzingatia kanuni za michezo.

Kwa upande wao, wanamichezo wa Utumishi SC wamemshukuru Mhe. Kikwete kwa kutenga muda wa kuwatembelea na kuwapa hamasa, wakieleza kuwa uwepo wake umeongeza morali na ari ya kuendelea kupambana katika hatua zinazofuata za mashindano.

Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora aliwapongeza wanamichezo wa Utumishi SC kwa hatua waliyofikia na kuwatakia kila la kheri katika michezo inayofuata, akiwataka kurejea na makombe. Aidha, amewahakikishia wanamichezo hao kuwa makombe yatakapowasili katika Mji wa Serikali, Mtumba, na kufikishwa ofisini kwake, wanamichezo wanaweza kutarajia zawadi kama sehemu ya kutambua juhudi na mafanikio yao.

 





















No comments:

Post a Comment