Na Lusungu Helela- Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philp Mpango, anatarajiwa kuzindua
Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma Disemba 11, 2024 katika eneo la
Njedengwa jijini Dodoma wenye lengo kutatua changamoto za makazi kwa watumishi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule
amebainisha hayo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari
kuhusu uzinduzi wa Mpango huo.
“Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma ulianza
kutekelezwa mwaka 2014 chini ya usimamizi wa Watumishi Housing Investments
(WHI) na hadi sasa, zaidi ya nyumba 1,000 zimejengwa katika mikoa 19
nchini Tanzania, ikiwemo Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Morogoro, Simiyu
Mtwara,”amesema Mhe. Senyamule
Aidha, amesema Mpango wa Makazi kwa Watumishi
wa Umma ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuboresha ustawi wa Watumishi wa
Umma, kuhakikisha wanapata makazi bora, yenye gharama nafuu na salama.
“Kupitia mpango huu, Watumishi wa Umma wanapata
fursa ya kumiliki nyumba kwa masharti nafuu, hatua inayolenga kuboresha hali ya
maisha na kuongeza ufanisi kazini.
“Aidha mpango huu unalengo la kuwawezesha wananchi
na hasa Watumishi wa Umma kiuchumi kupitia umiliki wa nyumba,”amesema Senyamule
Vilevile, amesema Watumishi Housing
Investments kupitia mpango huo imetoa mikopo yenye masharti nafuu kwa Watumishi
wa Umma ili kuwawezesha kumiliki nyumba kwa urahisi zaidi.
“Utekelezaji wa Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa
Umma ni dhamira pana ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata fursa ya
kumiliki makazi bora,”amesisitiza
Pia, amesema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, inawaalika
Watanzania wote kushiriki katika hafla hiyo muhimu ambayo inaashiria hatua
kubwa katika kuboresha maisha ya Watumishi wa Umma na maendeleo ya sekta ya
makazi nchini.
“Hafla hii si tu uzinduzi wa Mpango wa Makazi kwa
Watumishi wa Umma, bali pia ni fursa ya kuonyesha mshikamano wa kitaifa katika
kutatua changamoto za makazi na kuimarisha ustawi wa jamii,”amesema Mhe.
Senyamule.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na Waandishi
wa Habari leo jijini Dodoma kuhusu Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philp Mpango, kuzindua Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma
Sehemu ya Waandishi wa Habar leo jijini Dodoma wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule kuhusu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philp Mpango, kuzindua Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma
Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi
Housing Investment, Dkt. Fred Msemwa
akitoa ufafanuzi wa baadhi ya masuala ambayo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.
Rosemary Senyamule kuzungumza na Waandishi wa Habar kuhusu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philp Mpango kuzindua
Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma
No comments:
Post a Comment