Na: Mwandishi Wetu - Dodoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu amesema ajira ya kudumu Serikalini imekuwa ikisababisha watumishi wa
umma kuwa wazembe na kukaa
bila kufanya kazi wakiamini ikifika mwisho wa mwezi watapata mshahara jambo
ambalo ni kinyume cha Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.
Mhe. Sangu ametoa kauli hiyo leo Desemba 19,
2024 jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi cha siku tatu
cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.
Amesema masharti ya ajira ya kudumu na
mafao Serikalini kwa Watumishi wa Umma yanawaharibu watumishi ambapo
wamejikuta wakifanya kazi kwa mazoea bila kuchukuliwa hatua licha ya
kukiuka Sheria, Taratibu na Kanuni jambo ambalo linaweza kuisababishia serikali hasara kubwa.
Mhe.
Sangu amesema katika ziara aliyoifanya
kwenye baadhi ya mikoa amebaini changamoto hizo hasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo kuna baadhi
ya maeneo amekuta Watendaji wa Kata na Vijiji wakifanya kazi kama
miungu watu bila kuchukuliwa hatua za nidhamu licha ya kulewa asubuhi mpaka
jioni huku wananchi wakikosa huduma.
"Nimefika moja
ya eneo
ambalo Mtendaji wa Kijiji na
Kata analewa kuanzia asubuhi mpaka jioni siku zote za kazi, wananchi wanahitaji
huduma hawapati, ukimuuliza mwajiri anasema ndio kawaida yake tumeshamzoea, katika
utumishi wa umma hakuna mazoea ya namna hiyo
na haikubaliki hata kidogo,"
alisema Mhe. Sangu.
Pia, alizitaja changamoto nyingine alizokutana nazo
katika maeneo hayo kuwa ni uzembe , vitendo vya rushwa,
ulevi uliokithiri, kutoa lugha zisizofaa, unyanyasaji, uonevu na ubinafsi
hasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, kutopandishwa vyeo, kutolipa malimbikizo
ya mishahara, na suala la uhamisho.
Amesema, wamebaini kuwa changamoto zote hizo zimesababishwa na
watumishi wazembe, wabinafsi na wasiotaka kuwajibika kwa weledi katika utekelezaji wa
majukumu yao.
Akizunguzia changamoto ya uhamisho, Naibu
Waziri
huyo amesema kuwa
mtumishi anahamishwa zaidi ya mara sita ndani ya miaka saba, bila kulipwa madai yake ya uhamisho jambo ambalo
linasababisha malimbikizo makubwa ya madai ambayo halmashauri husika haiwezi
kuyalipa hivyo kuomba msaada Serikali Kuu na kuisababishia Serikali hasara kubwa.
"Unaweza
kukuta madai yanafikia robo
tatu ya mapato ya ndani ya halmashauri hivyo kusababisha ugumu wa kuyalipa, niwaase
mtekeleze majukumu yenu kwa waledi, mtumishi anapohamishwa hakikisheni analipwa kwa wakati
si kulimbikiza madai," amesistiza .
Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya
Rais (UTUMISHI), Bw.
Juma Mkomi akizungumzia utekelezaji
wa maagizo ya Waziri Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuhusu watumishi waliobainika
kughushi barua amesema,
tayari ameshachukua hatua na kuwaandikia barua waajiri wote kuzichunguza kwa siri barua zote wanazozipokea na
kubaini kama ni halisi kutoka Ofisi
ya Rais-UTUMISHI.
Katibu
Mkuu Mkomi amesema, zipo barua ambazo zinatengenezwa mtaani na
kuwekewa nembo ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI, hivyo katika kukomesha vitendo
hivyo visivyokuwa na maadili onyo kali linatolewa kwa wanaohusika na vitendo
hivyo na hatua zitachukuliwa dhidi yao.
Kikao kazi hicho kimewashirikisha Wakuu wa Idara za
Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara, Idara Zinazojitegemea,
Wakala za Serikali, Mashirika na Taasisi za Umma, Sekretarieti za Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Kaulimbi ya kikao kazi hicho ni “Kusimamia Sera na Sheria za Utumishi wa Umma Kupitia Mifumo ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala wa Kidijitali Iliyoboreshwa.”
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus
Sangu akizungumza
na Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa
Rasilimaliwatu (hawapo
pichani) wakati akifunga kikao kazi kilichofanyika kuanzia tarehe 17-19 Disemba,
2024 katika Ukumbi wa Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali Mtumba.
Baadhi ya Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu
wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu (hayupo pichani) wakati
akifunga kikao kazi
cha Viongozi hao kilichofanyika Ukumbi wa Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali
Mtumba.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deus Sangu (hayupo pichani) kuzungumza na kufunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu
kilichofanyika katika Ukumbi wa Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali Mtumba.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Idara na Vitengo kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu wakati akizungumza na Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu (hawapo pichani) wakati akifunga kikao kazi hicho kilichofanyika kuanzia tarehe 17-19 Disemba, 2024 katika Ukumbi wa Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali Mtumba.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akimkabidhi tuzo Mkuu wa Idara ya
Rasilimaliwatu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Bw. Abdulrahman Muya baada ya
taasisi hiyo kuwa mshindi wa pili usimamizi bora wa Rasilimaliwatu. Wa kwanza
kushoto ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi na wa kwanza kulia
ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Utumishi wa Umma, Bi. Felista Shuli.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu (katikati) akijiandaa kukabidhi tuzo kwa
washindi bora wa ofisi zilizosimamizi Rasilimaliwatu katika utendajikazi. Kulia
kwake ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi na kushoto
kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Utumishi wa Umma, Bi. Felista Shuli.
Baadhi ya Wakuu wa
Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu (hayupo pichani) wakati
akifunga kikao kazi cha Viongozi
hao kilichofanyika Ukumbi wa Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali Mtumba.
No comments:
Post a Comment