Tuesday, December 17, 2024

WAZIRI SIMBACHAWENE ATOA MAAGIZO KUMI YA KIMKAKATI KWA WAKUU WA IDARA ZA UTAWALA NA USIMAMIZI WA RASILIMALIWATU SERIKALINI

Na Mwandishi Wetu

Tarehe 17 Disemba, 2024

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ametoa maagizo 10 kwa Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini.

Maagizo hayo ni pamoja na kuzitaka Mamlaka za nidhamu kuchukua hatua stahiki na kwa wakati kwa watumishi wote waliobainika kuwa na barua za kughushi na walioshiriki katika mchakato wa kughushi barua za uhamisho kwa tarehe zilizobainishwa katika barua za maelekezo ikiwa ni pamoja na Waajiri kuacha kuwasilisha na kupitisha barua za maombi ya masuala mbalimbali ya kiutumishi ambayo kwa sasa yanashughulikiwa kupitia Mifumo.

Waziri Simbachawene, ametoa maagizo hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha kazi cha siku tatu kwa Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu chenye lengo la kuboresha utendaji kazi kwa Watumishi wa Umma Serikalini.

Amesema kwa nafasi walizonazo Wakurugenzi hao kwenye Taasisi wanazotoka ni jicho la Ofisi anayoingoza katika kusimamia utekelezaji wa Sera za Utawala, Maadili, Serikali Mtandao, Makazi ya Watumishi wa Umma, Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa na Usimamizi wa Rasilimaliwatu.

"Katika kutekeleza Sera tajwa hapo juu, mnawajibika kusimamia ukamilishaji wa taratibu za Ajira, mipango ya rasilimaliwatu, utendaji kazi, uendelezaji wa rasilimaliwatu na mifumo mbalimbali ya kiutumishi ambayo imesanifiwa kwa ajili ya kuwawezesha kutekeleza majukumu yenu. Mifumo hiyo ni pamoja na Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (e-Watumishi), 

Pia Mfumo wa Huduma kwa Watumishi wa Umma (ess) ambao una madirisha muhimu ya e-Utendaji, e-Uhamisho, e-Mikopo na e-Likizo. Vilevile, Mhe. Simbachawene amewafahamisha kuwa wana jukumu la kusimamia Maadili, nidhamu, utekelezaji wa Miundo na Mifumo ya uendeshaji wa utoaji huduma ili kuwa na Utumishi wa Umma wenye tija. 

Katika agizo lake la pili Waziri Simbachawene amemuagiza Katibu Mkuu, UTUMISHI kutoendelea kufanyia kazi maombi yote yanayowasilishwa katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora nje ya Mifumo iliyoanza kufanya kazi ili kuhakikisha Mifumo hiyo inatumika ipasavyo.

"Agizo langu la Tatu, nawaelekeza Waajiri wote kuhakikisha mnajiunga na kutumia kikamilifu Mifumo ya Kiutumishi na Uwajibikaji ambayo imesanifiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kuzinduliwa na Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa mnamo tarehe 23 Juni, 2024," amesema Mhe. Simbachawene.

Waziri Simbachawene katika agizo lake la Nne amewataka waajiri wote kuhakikisha wanasafisha taarifa za watumishi zilizopo katika Mfumo Jumuishi wa taarifa za kiutumishi na mishahara (e-Watumishi) kwa ajili ya kuwezesha utoaji uamuzi sahihi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi

"Agizo langu la Tano, nawataka Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wote mhakikishe mnasimamia utekelezaji wa Mifumo kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa mara kwa mara na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora," amesema Mhe. Simbachawene.

Mhe. Simbachawene katika agizo lake la Sita amewataka Waajiri kuwa wabunifu na kutafuta ufumbuzi ili mipango ya Taasisi zao isiathirike au kutotekelezwa kwa kisingizio cha kukosa fedha;

Pia, Waziri Simbachawene amewaagiza Waajiri hususani wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga nafasi za ajira mpya kwa kuzingatia maelekezo ya mwongozo wa maandalizi ya Ikama na Bajeti hususan kwenye maeneo ya rasilimaliwatu yenye upungufu mkubwa na ambayo ni kipaumbele ikiwa ni agizo lake la Saba.

Aidha katika agizo lake la nane, Mhe. Simbachawene amewaagiza Waajiri wote kuwapokea watumishi waliopangiwa vituo vya kazi au waliohamishiwa katika Taasisi zao pamoja na kuwachukuliwa hatua stahiki watumishi wenye utendaji kazi usioridhisha kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya utumishi wa umma.

Waziri ametoa agizo la Tisa na la Kumi akiwataka Waajiri wote kushughulikia ujazaji wa nafasi za uongozi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu na kuwaandaa watumishi wao na mabadiliko kwa kuwaandalia mafunzo yenye kukidhi matarajio ya nchi yetu, pamoja na mazingira yanayotuzunguka ili wakabiliane na mabadiliko yanayoendelea kwa kasi na teknolojia.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na Wakuu  wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu (hawapo pichani) wakati akifungua kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali Mtumba.


Baadhi ya Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati akifungua kikao kazi cha Viongozi hao kilichofanyika katika Ukumbi wa Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali Mtumba. Wengine ni Viongozi mbalimbali.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) kuzungumza na Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika kikao kazi cha Viongozi hao kilichofanyika katika Ukumbi wa Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali Mtumba.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi akitoa utambulisho wa Viongozi waliohudhuria kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu (hawapo pichani) kilichofanyika katika Ukumbi wa Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali Mtumba.

 

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Utumishi wa Umma, Bi. Felista Shuli akielezea malengo ya kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) kufungua Kikao kazi hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali Mtumba.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Idara na Vitengo wa ofisi hiyo mara baada ya kufungua kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kilichofanyika katika Ukumbi wa Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali Mtumba. Wengine ni Viongozi mbalimbali waliohudhuria ufunguzi huo.


Katibu Tawala Msaidizi-Utawala na Rasilimaliwatu-Singida, Bw. Stephen Pancras akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) baada ya Waziri huyo kufungua kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kilichofanyika katika Ukumbi wa Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali Mtumba.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu baada ya kufungua kikao kazi cha viongozi hao kilichofanyika katika Ukumbi wa Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali Mtumba. Wengine ni Viongozi mbalimbali waliohudhuria ufunguzi huo.


No comments:

Post a Comment