Saturday, October 26, 2024

WAZIRI SIMBACHAWENE: SERIKALI YATENGA SHILINGI BIL. 11 MABORESHO YA HOSPITALI YA AMANA

           Na Lusungu helela

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Tanzania imepokea Dola milioni 14.5 kutoka Ubalozi wa Korea Kusini, sawa na shilingi bilioni 38 ambazo zitagawanywa katika hospitali tatu ikiwemo Hospitali ya Rufaa Amana ambayo itapata kiasi cha shilingi bilioni 11 kwa ajili ya kuboresha ujenzi wa majengo ya huduma ya mama na mtoto.

 

Ametoa kauli hiyo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika harambee maalumu ya kuchangia ukarabati na ujenzi wa majengo ya watoto njiti na wajawazito iliyofanyika usiku wa kuamkia leo katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

 

Mhe. Simbachawene amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika Hospitali za Amana, Temeke pamoja na Mbagala katika kuhakikisha wajawazito  na watoto njiti wanapata huduma bora na kupunguza vifo wakati wa kujifungua.

 

Aidha amewashukuru wadau wote kutoka taasisi na mashirika mbalimbali kwa kujitoa katika harambee hiyo maalumu na kuwasihi watoe kwa moyo kwani Hospitali ya Amana ni kubwa na lazima yafanyike makubwa.

 

Kwa upande wake  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila amesema  katika harambee ya kuchangia ukarabarati na ujenzi wa majengo ya watoto njiti na wajawazito katika Hospitali ya Rufaa ya Amana  kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kimepatikana kutoka kwa wadau mbalimbali waliojitokeza kuchangia.

 

Ametoa wito kwa wadau na marafiki wa Hospitali ya Amana kuendelea kujitoa kwa hali na mali ili fedha zitakazopatikana ziweze kukamilisha majengo hayo 

 

Amewahakikisha wadau hao kuwa fedha itakayopatikana itatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza wakati wa  harambee maalumu ya kuchangia ukarabati na ujenzi wa majengo ya watoto njiti na wajawazito iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisalimiana na Rais wa Mabingwa wa Soka nchini, Yanga Afrika, Mhandisi Hersi Said mara baada ya kusema timu hiyo na mfadhili wake, Kampuni ya GSM itachangia kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kukarabati na kujenga majengo ya watoto njiti na wajawazito sambamba na ununuzi wa vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Amana 


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuzungumza wakati wa  harambee maalumu ya kuchangia ukarabati na ujenzi wa majengo ya watoto njiti na wajawazito iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

 


 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment