Wednesday, October 9, 2024

WAZIRI SIMBACHAWENE APOKEA VIKOMBE VYA USHINDI




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewapongeza Viongozi na wanamichezo wa Ofisi yake kwa kupambana na kutwaa vikombe viwili vya ubingwa katika michezo inayosimamiwa na Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI).

 Mhe. Simbachawene ametoa pongezi Oktoba 8, 2024 wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika Jengo la Ofisi za Utumishi, Mtumba jijini Dodoma kwa lengo la kupokea Vikombe vya ushindi katika mchezo wa mpira wa miguu na mashindano ya baiskeli ya SHIMIWI. 

"Niwapongeze kwa kuleta heshima kubwa katika Ofisi hii, ubingwa wa mpira wa miguu na ushindi wa nafasi ya kwanza kwenye mashindano ya baiskeli unadhihirisha dhamana yetu ya kusimamamia Watumishi wa Umma na kuwa mfano kwa kila jambo lililo jema" alisema Mhe. Simbachawene.

 

Amesisitiza kuwa, ushindi wa vikombe viwili ni hatua kubwa lakini kubwa zaidi ni kitendo cha kubeba kombe la mpira wa miguu. Kombe la mpira wa miguu linaleta maana zaidi kuliko waliochukua vikombe vingine.

 Aidha, Mhe. Simbachawene ametumia fursa hiyo kumpongeza Katibu Mkuu-UTUMISHI Bw. Juma Mkomi kwa kuwa chachu ya kuimarisha michezo Ofisini amemuomba kuendelea kuwa na ari hiyo ili kujenga afya njema za watumishi mahala pa kazi. 

 Naye Naibu Waziri Mhe. Sangu amewapongeza wanamichezo hao kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kupambana ili kufikia malengo yaliyokuwa yamewekwa ya kuleta ushindi.


Amesema kuwa, ushindi huo wa vikombe viwili unatokana na jitihada kubwa zilizofanywa na Katibu Mkuu, Bw.Juma Mkomi ya kuwa karibu na wachezaji hao na kuwapa hamasa na zaidi kuwawezesha ipasavyo. 

 Halikadhalika, ametoa pongezi za kipekee kwa Bw. Mkomi kwa kuwa kiungo muhimu sana kwa watumishi wa Ofisi hiyo, mathalani ukaribu wake kwa wachezaji umekuwa chanzo cha kufanya vizuri kwenye michezo ya SHIMIWI na ameombwa kuendelea kuwa na moyo huo ambao matokeo yake yanaonekana kwa kila mmoja mtumishi.

 Naye Katibu Mkuu Mkomi amewapongeza wachezaji hao huku akimshukuru Waziri Mhe. Simbachawene pamoja na Naibu Waziri Mhe. Deus Sangu kwa ushirikiano wao mkubwa walionao katika kupenda na kuthamini michezo. 

 "Nakushukuru Naibu Waziri Mhe. Sangu kwa kufika katika kambi za mashindano hayo na kutoa hamasa kubwa wa watumishi wetu, hamasa hiyo imeleta ushindi ambao tunafurahia hii leo” alisema Bw. Mkomi 

 Mashindano ya SHIMIWI yalihitimishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora  Oktoba 5, 2024 Mkoani Morogoro.

 



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo Mhe. Deus Sangu pamoja na Katibu Mkuu, Bw. Juma Mkoni wakipokea vikombe kutoka kwa baadhi ya wachezaji wakati wa hafla fupi ya kupokea vikombe hivyo.

 






Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo Mhe.Deus Sangu  pamoja na Katibu Mkuu, Bw.Juma Mkoni wakiwa kwenye picha pamoja na baadhi ya Wachezaji wa mpira wa miguu pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi hiyo wakati wa hafla fupi ya kupokea vikombe hivyo.





Baadhi ya Wachezaji wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vikombe vya Mashindano ya SHIMIWI.

 

 

 

 

 

 

 

 


No comments:

Post a Comment